WATU wawili wamekufa katika matukio mawili katika Mkoa wa Katavi,
likiwemo la mtoto wa kike wa umri wa miaka tisa aliyeuawa kwa
kucharangwa mapanga na watu wasiofahamika baada ya kumnajisi kwa zamu.
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama, Paza Mwamlima ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humu
kuhakikisha linawasaka na kuwatia mbaroni watu wasiofahamika ambao
wanadaiwa kumnajisi na kumuua mtoto huyo.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa mkasa huo ulitokea Aprili
14, saa 6:00 mchana katika kijiji cha Kapanga wilayani humu baada ya
mtoto huyo kuagizwa na babu yake, Maela Mayanga (58) kwenda shambani ili
akafukuze tumbili waliovamia kijiji hicho wanaokula mahindi yaliyopo
shambani.
Inadaiwa kuwa mtoto huyo baada ya kulinda tumbili wasile mazao
shambani kwa muda mrefu ndipo babu yake alipomwagiza kaka wa mtoto huyo
aende shambani ili mtoto huyo arudi nyumbani kwa ajili ya chakula.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa shamba la mzee Mayanga halikuwa mbali na
kijiji hicho. Inaelezwa kuwa kaka huyo alipofika shambani hakumwona dada
yake, hata alipomwita kwa kupaza sauti hakuitikiwa, ndipo akaanza
kumtafuta akiamini alikuwa amejificha na anacheza mchezo wa kujificha.
“Lakini baada ya kutafuta kwa muda mrefu alikata tamaa na kurejea
kutoa taarifa nyumbani kuwa hakumwona dada yake huyo,” alieleza mtoa
taarifa.
Baadhi ya mashuhuda kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini
walieleza kuwa baada ya mzee Mayanga kupata taarifa hiyo aliambatana na
mjukuu wake huyo wa kiume, walienda shambani ambapo walimtafuta kwa muda
mrefu bila mafanikio hivyo wakakata tamaa wakirejea kijijini.
Kwa mujibu wa Mzee Mayanga, aliamua kwenda na mwalimu wa dini wa
Kanisa Katoliki kijijini humo ambaye aligonga kengele ambapo waumini wa
kanisa hilo wakakusanyika kwa wingi.
Mzee Mayanga aliwasimulia kisa chote ndipo kundi kubwa la waumini hao
walielekea shambani na kuanza kumsaka mtoto huyo kwa zaidi ya saa tatu
ndipo waliupata mwili wa mtoto huyo ukiwa umetupwa kando ya mto karibu
na mashamba ya kijiji hicho.
Baada ya kuukagua mwili huo ilibainika kuwa mtoto huyo alinajisiwa
kwani alikuwa amechanika vibaya sehemu za siri akiwa na majeraha makubwa
kifuani. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Rashid Mohamed alikiri
kutokea kwa tukio hilo, akiapa kuwa Polisi itafanya kila liwezekanalo
ili watuhumiwa wakamatwe na hatua za kisheria zichukue mkondo wake.
Katika tukio lingine lililotokea Aprili 13, mwaka huu saa 5:00 usiku,
Shukuru Korongo (32) ameuawa kwa kupigwa na rafiki yake Pisikitu Maiko
(30), wakigombea viroba vya pombe kali iitwayo Zed katika sherehe
iliyofanyika kwa jirani yao katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alieleza kuwa
wakati marafiki hao walipokuwa wakinywa pombe hiyo kali, Maiko aliwahi
kumaliza na alimuomba Shukuru amgawie viroba vya pombe hiyo kali