ASKARI wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Sajenti Ally Salum maarufu Kinyogori, ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake Mkuranga mkoani Pwani.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi, imesema kuwa mauaji hayo yalifanyika juzi saa 1.30 jioni katika Kijiji cha Chatembo, Kata ya Mwandege wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Katika taarifa hiyo, Kamanda Mushongi alisema watu wawili wakiwa wamevaa makoti meusi na kuficha sura zao, waliingia ndani ya uzio wa nyumba ya askari huyo wakiwa katika usafiri wa pikipiki aina ya Boxer.
Alisema katika tukio hilo, wauaji hao hawakuchukua kitu chochote zaidi ya ufunguo wa gari ambalo hata hivyo hawakulichukua.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali wa waliohusika na limeomba ushirikiano kutoka kwa wananchi wenye taarifa zitakazosaidia wahusika kukamatwa kwa haraka.
Kamanda Mushongi alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam na utakabidhiwa kwa ndugu zake kwa mazishi mara baada ya kufanyiwa uchunguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Simon Sirro alisema tayari Jeshi la Polisi linawashikilia watu 14 wakihusishwa na tukio hilo.
“Waliofanya tukio hilo hata waende wapi watakamatwa tu, hili ni tukio la Mkoa wa Pwani lakini kwasababu alikua anafanya kazi katika mkoa wangu taarifa hizo ninazo,” alisema Kamanda Sirro.
Kamanda Sirro alisema tangu juzi Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi na oparesheni mbalimbali na wanaendelea kupokea taarifa kutoka kwa watu mbalimbali kuhusu tukio hilo.
 
Top