PENGINE hii ni habari mpya kwa baadhi ya watu. Ni kwamba, wakati ikifahamika na wengi kuwa matunda ya matikiti maji ni kiburudisho safi kitokanacho na maji yake matamu, imebainika kuwa mbegu za matunda hayo zina faida zaidi ya sita kwa wanandoa
Ukweli huo umebainika kutokana na uchunguzi uliofanywa na Nipashe, ukihusisha mahojiano ya kina na baadhi ya walaji wa mbegu hizo, madaktari na pia kupitia ripoti mbalimbali za masuala ya lishe.
Katika uchunguzi huo, imebainika kuwa mbegu za matikiti huimarisha afya ya uzazi ya wanandoa, hasa kina baba, na hivyo kuwa na fursa kubwa ya kuongeza furaha baina ya wapendano.
Aidha, faida ya pili mwilini kati ya nyingi zitokanazo na ulaji wa mbegu za matikiti ni kwa wahusika kupunguza uwezekano wa kukabiliwa na shinikizo la damu; tatu kusaidia mmeng’enyo wa chakula; nne kuongeza mafuta yasiyokuwa na lehemu; tano kuipa afya mishipa ya fahamu na sita, ni kuimarisha afya ya ngozi.
“Faida zipo nyingi sana mwilini kwa walaji wakiwamo wanandoa, na yote hayo yanatokana na ukweli kwamba mbegu za matikiti zimejaaliwa kuwa na viinilishe vingi sana…. kuna protini, vitamin na madini mengi yakiwamo ya chuma, zinc, shaba, potassium, magnesium, phosphorous, sodium na manganese,” mmoja wa madaktari aliiambia Nipashe na kuongeza:
“Ni vizuri watu wakajenga desturi ya kula mbegu za matunda haya (matikiti maji). Zina manufaa mengi mwilini… hata kina baba wanaweza kujiongezea heshima nyumbani kwa kujenga mazoea ya kula mbegu hizo.”
Akizungumza na Nipashe, Daktari Seileman Hassan wa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, alisema ni kweli zipo tafiti nyingi zinazothibitisha kuwapo kwa faida kubwa mwilini ya ulaji wa mbegu za matikiti maji.
Alisema vilevile kuwa ni kweli mbegu hizo zitokanazo na tunda la matikiti lenye kiwango cha maji kwa wastani wa asilimia 92, zina uwezo wa kuimarisha ndoa kwa walaji.
Dk. Hassan alisema katika baadhi ya ripoti, imethibitika kuwa kuwa mbegu hizo zina asilimia 74 ya madini ya manganizi, asilimia 57 ya phosphorosu, asilimia 48 ya magnezium, asilimia 48 ya shaba, asilimia 23 ya zinc, asilimia 20 ya protini na asilimia 16 ya chuma, vyote vikiwa ni virutubisho muhimu mwilini mwa kila mwanadamu, wakiwamo wanandoa wenye nia ya kuongeza furaha katika mahusiano yao ya kiunyumba.
“Vitu hivi ni muhimu kwenye mwili wa binadamu na uzuri ni kwamba ulaji wa mbegu hizi humwezesha mtu kuvipata vyote kwa wakati mmoja,” alisema Dk. Hassan na kuongeza:
“Mitaani watu huangalia faida moja tu ya ulaji wa mbegu za tikiti, nayo ni suala la kuongeza hamu ya kufanya tendo la ndoa. Hilo lina ukweli wake kutokana na madini yaliyomo kwenye mbegeu hizi… lakini sisi (watu wa afya) tunakwenda mbali zaidi.
Hatuangalii tu uwezo wa kuamsha hisia za mapenzi, bali pia faida nyingine ikiwa ni pamoja na uwezo wa mbegu hizo kuupa mwili na ubongo nguvu na kuimarisha pia maeneo mbalimbali mwilini.”
Aidha, Dk. Hassan alisema ulaji wa mbegu hizo, pamoja na tikiti lenyewe, huwa na uwezo pia wa kuondoa vijisumu mwilini na kuzuia uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa mbalimbali kama ya saratani.
Alisema ingawa bado kuna tafiti mbalimbali zinaendelea kufanyika na hasa nchini Marekani, lakini utafiti wa awali umeonyesha kuwa mbegu za tikiti zina uwezo wa kuwasaidia kwa kiasi kikubwa watu wenye kisukari na pia kuimarisha mifumo ya figo.
Aidha, alisema Shirika la Afya Duniani (WHO) limependekeza ulaji wa tunda hilo kwa sababu humsaidia mtu kupata vitu vingi muhimu kwa wakati mmoja.
Kuhusiana na jinsi ya kuzitumia ili kupata matokeo bora, Dk. Hassan alisema ni vyema walaji wakazitafuna wakati wakila tikiti lenyewe au kuzila baada ya kuziponda zilainike bila ya kuharibu ubora wake.
“Muhimu kuzingatia ni kwamba kuzimeza mbegu hizo bila kuzitafuna hakutaleta faida yoyote mwilini…ni kwa sababu baadaye zitatoka kwa njia ya haja kubwa kama zilivyomezwa. Hivyo ni lazima ziwe zimetafunwa na mlaji au ziliwe wakati zikiwa zimesagwa,” alisema.
Daktari Amani Assey, ambaye ni mtaalamu wa mambo ya lishe, aliungana na maelezo ya Dk. Hassan kwa kusema kuwa ulaji wa mbegu za tikiti maji huleta faida kwa wote, yaani kina baba na kina mama.
Akizungumzia kwa kina mama, alisema mbegu za matikiti husaidia husaidia kusafisha mfumo wa uzazi na kwa kina baba, mbegu hizo hurutubisha mbegu za kiume na kuzifanya kuwa imara na zenye ubora zaidi.
“Na kwa wale wenye majipu, mbegu hizi ni dawa kwao kwa sababu hukusanya uchafu wa majipu mwilini,” alisema na kuongeza.
“Watu wengi wanapokula tikiti huziondoa mbegu zake bila kujua faida zake mwilini… lakini zina faida nyingi kwa afya na hivyo ni bora kuzitafuna kumeza.”

MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA

    TANGAZO
http://studentswagas.blogspot.com

 
Top