WATU watano wamekufa baada ya basi aina ya Super Sami, mali ya
Kampuni ya Super Sami lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza,
kugonga jiwe na kupinduka katika barabara ya Mwanza-Shinyanga eneo la
Mabuki wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
Basi hilo lenye namba za usajili T499 BCB, likiendeshwa na dereva
William Elias maarufu kama Massa (44) ambaye ni mkazi wa Mabibo jijini
Dar es Salaam, lilipata ajali hiyo saa saba usiku wa kuamkia jana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema baada ya
kugonga jiwe dereva alishindwa kulimudu na kupinduka na kusababisha vifo
vya watu watano akiwemo dereva, msaidizi wake na majeruhi 13.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva aliyekuwa kwenye mwendokasi
hali iliyosababisha basi hilo kugonga jiwe lililokuwa barabarani na
kushindwa kumudu basi hilo lililoserereka na kupinduka.
Aliwataja waliokufa kwenye ajali hiyo kuwa ni Massa ambaye ni mkazi
wa Dar es Salaam, Vaileth Odede (21) mkazi wa Mwanza, mwanamume mmoja na
wanawake wawili wenye umri kati ya miaka 25-30 ambao hawajatambulika.
“Majeruhi watano kati ya 13 wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya
Bugando kupatiwa matibabu, na wengine wanane wanatibiwa katika Hospitali
ya Wilaya ya Misungwi,” alisema Kamanda Msangi.
Aliwataja majeruhi wanaoendelea na matibabu katika Hospitali ya
Misungwi kuwa ni Sophia Miraji (25), Kibilo Mwacha anayekadiriwa kuwa na
miaka kati ya 35 hadi 40, Boniphace Charles (38-40) na Frank Munyuni
(30).
Majeruhi wengine ni Stanley Zacharia (25), Sia Dauson (28), Hellen
Luheke( 30-35), Michael Leonard (30-35), Kudra Ibrahim ambaye ni mtoto
wa miaka miwili na miezi 10, Zamda Issa (24), Marietha Christopher (26),
Elizabeth Simon (40) na Dickson Msamba (22).