Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Simon Haule
MFANYABIASHARA wa ng’ombe, William Clement (54) mkazi wa Kijiji cha
Ihanja Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, ameuawa kwa kuchinjwa shingo
kutokana na kumdai mtu mmoja wa kijiji cha jirani Sh 400,000.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Simon Haule alisema mauaji
hayo yametokea Juni 22, mwaka huu ambako Clement aliaga nyumbani kwake
saa 1.30 usiku kuwa anaenda kwa Hassan Abdallah (38) wa Kijiji cha Mpetu
wilayani humo kumdai deni lake la Sh 400,000.
Haule alisema ilipofika saa 5:35 usiku, mfanyabiashara huyo alituma
ujumbe mfupi wa simu kwa mtoto wake aitwaye Faraja kumjulisha kuwa
alikuwa anarejea nyumbani lakini kulikuwa na watu waliokuwa wanataka
kumdhuru hivyo akamtaka aende haraka kumsaidia.
Alisema kwa bahati mbaya Faraja hakuuona ujumbe huo hadi kesho yake
ambako alitoa taarifa kwa majirani na msako mkali wa kumtafuta ulianza
mara moja na mwili wa marehemu kugundulika ukiwa umefichwa chini ya
daraja katika Barabara ya Iseke – Ihanja katika Kijiji cha Iseke.
Kaimu Kamanda alisema tayari Polisi imeshamkamata mtuhumiwa, Hassan
Abdalllah na kwamba baada ya mahojiano atafikishwa mbele ya mahakama ili
kujibu shitaka linalomkabili.