ASKARI wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Raphael Makongojo (25)
aliyembaka aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya
Korogwe amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Pia Makongojo amepewa adhabu kali, ikiwemo viboko 12 pamoja na
kuamriwa kutoa faini ya Sh milioni 15 mara atakapomaliza kifungo chake.
Hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Arusha ndani ya
chumba cha faragha (chemba) ambako waandishi hawakuruhusiwa kusikiliza
hukumu, lakini baadaye waliambiwa kwa sharti la hakimu wala waendesha
mashtaka kutajwa majina yao kwa sababu kesi hiyo iliendeshwa faragha.
Awali kesi hiyo ilianza kwa mshitakiwa kusomewa maelezo yake ya awali
akituhumiwa kumbaka mwanafunzi wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari
ya Wasichana ya Korogwe ambaye hivi sasa amemaliza masomo.
Awali askari huyo alishushwa pamoja na mahabusu wenzake mahakamani
hapo, lakini kwa kuwa kesi inayomkabili ni ya ubakaji hivyo inasikilizwa
ndani ya chumba cha faragha (chemba) ambako hakuna ruhusa kwa
wanahabari kuandika habari hiyo hadi hapo hukumu itakapotolewa.
Kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria Namba 186 (3) cha Sheria ya Mwenendo
wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 ya Mwenendo wa Makosa ya Kujamiiana ya
Mwaka (1998) inayosema kuwa bila kujali masharti ya sheria nyingine
yoyote inayohusisha makosa ya kujamiiana, ushahidi au mashahidi
watakaohusika hawaruhusiwi kutolewa kwenye chombo chochote cha habari.
Awali, mshitakiwa huyo kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani hapo
na kusomewa shtaka lake kwa hakimu (jina linahifadhiwa) ambako Wakili
wa Serikali (jina linahifadhiwa) alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa
huyo alitenda kosa hilo Januari 16, mwaka huu katika eneo la Kwa Mrombo,
FFU jijini hapa.
Alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu cha
130(1 na 2 a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 16.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa, mama mzazi wa mtoto huyo ambaye
hakupenda kutaja jina lake, aliiomba serikali kuingilia kwa makini
sheria inayohusu makosa ya ubakaji ili adhabu itakayotolewa kwa mbakaji
iwe kifungo cha maisha badala ya hakimu au mahakama kutoa kifungo cha
miaka 30.