DEREVA teksi mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, Ally Mzako (29) amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mtoto mwenye umri wa miaka mitano.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Flora Haule kutokana na kukamilika kwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashitaka ambao ulikuwa na mashahidi wanne pamoja na virlelezo vya daktari.
“Kutokana na ushahidi uliowasilishwa, Mahakama inakutia hatiani kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka mitano ili iwe fundisho kwa wote wenye tabia chafu za kubaka watoto na watambue kuwa sheria ipo na inafanya kazi,” alisema Hakimu Haule.
Awali, katika utetezi wake kwa nini asipewe adhabu kali, Mzako alidai kupunguziwa adhabu na kukana hakutenda kosa hilo.
Upande wa Mashitaka kwenye kesi hiyo namba 237 ya mwaka 2014 ulikuwa na mawakili wawili, Esther Kyara na Chesense Gavyole ambao waliiambia mahakama hiyo kuwa hakukuwa na rekodi za mashitaka ya nyuma dhidi ya mshitakiwa.
Katika ushahidi, inadaiwa kuwa siku ya tukio, Julai 19, 2014, Mzako alikodiwa na mama wa mtoto huyo kwa ajili ya kumpeleka Hospitali kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya uzazi, ambapo ndani ya teksi hiyo kulikuwa na mtoto huyo aliyebakwa.
Inadaiwa anasema kuwa wakati wakienda hospitali, mama wa mtoto huyo alimuomba, Mzako asimamishe gari kwa ajili ya kuingia kwenye duka la kubadilishia fedha na kumwacha akiwa na mtoto wake huyo ndani ya gari.
Inadaiwa pia kuwa mara baada ya mama huyo kurejea mahali alipowaacha, Mzako na mwanaye, alikuta teksi hiyo haipo mpaka baadaye alipomkuta mtoto wake huyo kwenye mazingira yaliyomtatanisha huku akiwa ameumizwa vibaya sehemu za siri.
Kwa mujibu wa vipimo vya daktari, mtoto huyo alikuwa amenajisiwa na kuondolewa usichana wake. Mzako alikiri kuifahamu familia hiyo na kuwatambua wateja wake hao wa zamani mara.

 
Top