WATU wawili wamefariki dunia jijini Dar es Salaam katika matukio tofauti
likiwemo la muuza magazeti Abel Damas, mkazi wa Kinondoni mtaa wa Togo
kujinyonga kwa soksi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema kifo hicho
kilitokea juzi saa moja asubuhi baada ya mwili wa Damas kukutwa kwenye choo cha
nyumba alimokuwa akiishi.
Kamanda Wambura alisema watu wa karibu na marehemu huyo walidai kwamba
alikuwa na anavuta bangi huku wakifichua kwamba Julai 11 mwaka huu alikwenda
katika Kanisa la TAG ili aombewe aache tabia hiyo.
Alisema mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika tukio jingine, mtembea kwa miguu mkazi wa Tegeta, Mathias Athanas
aliyekadiriwa kuwa na umri kati ya 45 hadi 50 alifariki dunia baada ya kugongwa
na gari.
Kamanda Wambura alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa nne usiku katika
barabara ya Bagamoyo eneo la Skaska ambapo gari lenye namba za usajili T293 CAH
Scania, ilililokuwa likiendeshwa na mtu asiyefahamika kumgonga Mathias.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya taifa Muhimbili
huku jitihada za kumtafuta aliyekimbia baada ya ajali zinaendelea.