Ghati Sagire ambaye licha ya umri wake kuwa mdogo, lakini sasa ni mke wa mtoto mwenzake. 


Kwa ufupi
  • “Walioana wakiwa na umri wa miaka 14 mwaka jana”


Ni muda wa saa 5:45 asubuhi tunafika nyumbani kwa  Simioni  Sagire, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mifugo katika kijiji cha Kwitete kata ya Nyamoko wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara.

Haikuwa kazi rahisi kufika kwenye mji huo, kutokana na kutokuwepo barabara ya kupita gari, inatulazimu kuacha gari na kutembea kwa miguu kwa dakika 45, kutokana na mazingira hayo.

Tunalakiwa na mama mmoja na binti mdogo akiwa amefunika kichwa chake kwa kitambaa cha mezani  kilichofumwa kwa nyuzi, uso wake ukiashiria kuwa anakitu kimemtokea, wakati wa kutusalimia anaonyesha kukunja uso ikiwa ni ishara kuwa anakabiliwa na maumivu makali, lakini pia amejaa hofu.

Hofu hiyo haikuwa kwa binti huyo tu bali hata mama aliyetulaki na  waliokuwepo hapo jirani, kwa kifupi ilitosha kuakisi kuwa kuna kitu kisichokuwa cha kawaida kimetokea ndani ya mji huo, walipata ujasiri kwa kuwa tulikuwa na Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, anawaita kwa lugha ya Kikurya, wanaitikia kwa lugha hiyo hiyo.

Kwa nini tupande milima na kushuka mabondeni
Kuzagaa kwa taarifa za vitendo vya ukatili  katika mji wa Mugumu aliofanyiwa mtoto  wa kike baada ya  kukatwa nyuma ya shingo kwa panga na kunusurika kufa, ndiyo msukumo wa kupanda milima na kushuka mabondeni.

Kumbe ni mke wa mtu
Mama aliyetupokea anaketi jirani yetu na kujitambulisha kwa majina ya Rhobi Simioni (46) mke wa Simioni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mifugo, tunamwomba atuitie mtoto wake aliyefanyiwa ukatili, kwa mshangao anasema, ”huyo ni mke wa mtoto wangu toka wameoana wana zaidi ya mwaka mmoja,”anasema na kutushangaza.

Anatambua mshangao wetu, kabla hatujasema kitu anamwita huyo mke wa kijana wake, anakuja kwa aibu na hofu lakini pia anahisi maumivu makali kutoka na shambulio lililolenga kumtoa roho.

Anajitokeza mtoto aliyekuwa amejifunika kitambaa kichwani, tunabaki kutizamana, lakini yeye bila hata chembe ya aibu anamtaka akae kwenye kigoda kisha aseme nasi kuhusiana na maswahibu yaliyomkuta.

Kabla hajasema kitu anatoa kitambaa kichwani na kutuonyesha shingo yake kwa nyuma,tunastushwa na hali hiyo, kisha anakaa na kujitambulisha kuwa anaitwa Ghati Sagire (15) mke wa Sagire (15)mtoto mwenzake ambaye sasa anaishi kwa kujificha akihofia kukamatwa kutokana na kumkata mke wake kwa panga.

Kisa ng’ombe walipigana malishoni



 
Top