Spika wa bunge la Embu nchini Kenya amepatikna baada ya
kutekwa nyara yapata siku nne zilizopita.
Bwana Justus Kariuki Mate alipatikana hoi na wafanyi
biashara wa kuuza mboga katika eneo lenye baridi kali la Limuru viungani mwa
mji mkuu wa Nairobi.
Spika huyo amekuwa mstaari wa mbele kuongoza juhudi za
kumng'oa mamlakani gavana wa jimbo la Embu Martin Wambora.
Wafuasi wake wakiongozwa na naibu wake Ibrahim Swaleh pamoja
na seneta wa jimbo hilo Lenny Kivuti walimtembelea hospitalini ambako amelazwa
ilikupata matibabu .
Spika huyo aliwaambia wafuasi wake kuwa ndio kwanza mkoko
umealika maua Embu kwani ataendelea na juhudi za kupalia na kukuza demokrasia .
Spika huyo anakabiliwa na madai kuwa alipuuza maagizo ya
mahakama ya kusitisha mswada wa kumng'oa Mamlakani gavana wa Embu kwa kukiuka
maadili ya ununuzi wa bidhaa na huduma za umma nchini kenya.
Spika huyo aliruhusu mjadala huo kuendelea mbele licha ya
makataa ya korti.
Afisa mmoja wa kitengo cha jinai Nicholas Muriuki Kangangi
alifikishwa mahakamani kwa dai ndiye aliyemteka nyara Spika huyo wa Bunge
alipokuwa katika mkutano na washika dau mjini Nairobi.
Polisi wamesema wanaendelea kuchunguza tukio hilo
linalotishia kuenea kwa demokrasia nchini Kenya.