Tukio hili la kusikitisha na kushangaza limetokea mkoani
Kagera, wilayani Muleba katika kijiji cha Bisole, ambapo mtu mmoja anayedaiwa
kuwa ni mganga wa kienyeji, Mujingwa John (20) ametiwa mbaroni kwa tuhuma za
kufanya mauaji ya mtoto Fausta Geofrey (8), na kumkata viungo vyake vya mwili
kisha kumzika chini ya kitanda chake.
Kufuatia kutokuonekana kwa mtoto huyo, wananchi wa kijiji
Cha Bisole waliungana kufanya msako, ambapo walifanikiwa kumkamata Mujingwa
John ambaye ni mganga wa kienyeji akiwa katika harakati za kubanika viungo vya
mtoto ambavyo amevikata baada ya kufanya mauaji.
Baada ya mahojiano na polisi mtuhumiwa, Mujigwa John (20)
amekiri kutenda tukio hilo la kinyama mnamo tarehe 21 mwezi Mei mwaka huu
majira ya asubuhi katika kijiji cha Bisole. Amesema kuwa alimkamata mtoto huyo
akiwa na wenzake wakielekea shuleni. Baada ya kumkamata alimvuta hadi nyumbani
kwake huku akiwa amemkaba, ambapo alimnyonga hadi kufa, kisha akamkata ngozi ya
mgongoni, mikono kwa kuanzia mkono wa kushoto huku akidai kuwa una bahati,
sehemu za siri na masikio ya mtoto huyo.
Mujigwa John aliendelea kueleza kuwa, uganga huwo aliurithi
kutoka kwa babu yake tangu alipokuwa na umri wa miaka 8, na hakupata fursa ya
kwenda shule katika maisha yake. Amesema kuwa tukio hilo lilikuwa ndio tukio
lake la kwanza na hakuwahi kufanya kabla.
Ameeleza kuwa dawa ambayo angeitengezeza kwa kubanika viungo hivyo
alivyo vikata kutoka mwilini mwa mtoto
huyo, angeiuza kwa wateja wake waliokuwa wakitafuta utajiri na bahati
kwa gharama ya shilingi za kitanzania 500 kwa ujazo wa kijiko kimoja.
Alipohojiwa kuhusu mtu aliyemtuma kufanya kitendo hicho,
alieleza kuwa hakuna mtu aliyemtuma bali alikuwa ameoteshwa na mizimu yake,
ambapo alitakiwa kumuua mtoto na kumkata viungo kwaajili ya kuchanganya na dawa
zake.
Ofisa mtendaji wa kijiji cha Bisole, Hamis Hassan, amekiri
kutokea kwa tukio hilo na alieleza kuwa baada ya mauaji hayo mtuhumiwa
aliufukia mwili wa mtoto huyo chini ya kitanda chake kisha kuweka nyasi juu
kuzuia watu wasigundue kama mahali hapo pamechimbwa.
___________________________________________________________________________________________________