UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kupitia kwa Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, umeweka
bayana kwamba Rais Jakaya Kikwete, ‘kupitia mlango wa nyuma’ anaunga mkono
juhudi zao.
Viongozi wa UKAWA ambao unatetea mapendekezo ya Rasimu ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokwishakuwasilishwa Bunge la Katiba na Jaji
Joseph Warioba, kwa sasa wanaendelea na mikutano yao ya kuhamasisha wananchi
kupinga juhudi za kuvuruga mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hasa
kuanzishwa kwa muundo wa Muungano wenye Serikali tatu.
UKAWA wanadai wameanza kufanikiwa katika harakati zao hizo
za uhamasishaji, kiasi cha baadhi ya wananchi kuwachangia fedha kwenye mikutano
ya hadhara, ili kuendelea na wajibu wao huo wa uhamasishaji.
Akizungumza na Raia Mwema baada ya kufanya mikutano ya
hadhara katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Mara, Dk.
Slaa alifafanua ni kwa namna gani Rais Kikwete anawaunga mkono kwa ‘mlango wa
nyuma’.
“Rais Kikwete amesaini Rasimu ya Warioba ukurasa wa mwanzo
na ameandika jina lake ukurasa wa mwisho, jambo ambalo kwa kawaida kwenye
michakato ya Katiba halitakiwi.
“Rais hatakiwi kusaini chochote, tofauti na sheria za
kawaida ambazo hadi Rais aridhie. Kwa sababu Katiba si ya rais bali ni ya
wananchi.
“Ukitaka kutafiti...angalia Katiba ya mwaka 1977, kwenye
nakala halisi, unakuta orodha ya majina ya wabunge waliopitisha ndiyo yanawekwa
kwenye Katiba.
“Akubali wazi wazi (Kikwete) ushauri wetu. Amesaini Rasimu
ya Warioba, hicho ndicho kitanzi kinachomnyonga. Jina lake limeandikwa kwenye
rasimu halafu anafika bungeni anaikana. Ndiyo maana tunamshitaki kwa
wananchi. Alichokifanya ni usanii na
kuwahadaa Watanzania na kama kweli hakuwa anakubaliana na Serikali tatu kwa
nini aliitisha Bunge na kuacha fedha za umma zinatumika kuliendesha Bunge hilo
la Katiba,” alihoji Dk. Slaa.
Aliongeza Dk. Slaa: “ Ni sawa na mama kutunza ujazito na
inapofikia muda wa karibu ya kujifungua....miezi tisa anatoa ujauzito huo. Rais
asingesaini tusingekuwa na nguvu ya kutamka hivyo. Amesaini, ameweka jina lake.
Alikuwa anajua.
“Bahati mbaya kwa kauli yake ndani ya ukumbi wa Bunge
ameanzisha vita ya kisiasa. Tunamwambia vita hii ya kisiasa hawezi kushinda kwa
sababu anapiga ngumi kwenye jiwe.
“Jiwe ni wananchi waliotoa maoni kwenye rasimu ya kwanza na
rasimu ya pili iliyowasilishwa katika Bunge la Katiba na Jaji Joseph Warioba.”
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa amesisitiza kama ilivyo kwa
viongozi wenzake wa UKAWA akiwamo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Profesa
Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wanachi (CUF)
na James Mbatia (NCCR- Mageuzi) kwamba hawatarejea kwenye Bunge la
Katiba iwapo CCM itaendelea kupinga mapendekezo ya Serikali tatu na Rasimu ya
Jaji Warioba kwa ujumla wake.
Lakini wakati viongozi hao wa UKAWA wakiwa na msimamo huo
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CC-CCM) Stephen Wassira ambaye pia
ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Uratibu na Uhusiano, Stephen Wassira wiki
kadhaa zilizopita aliwahi kutoa kauli tata kuhusu UKAWA.
Katika kauli yake hiyo iliyotafsiriwa na baadhi ya vyombo
vya habari nchini kuwa ni kitisho, Wassira alisema UKAWA wasiporejea kuendelea
na mjadala wa rasimu ya Katiba katika Bunge la Katiba basi, hakutakuwa na namna
nyingine zaidi ya kubadilisha kanuni ili kazi ya kuandika Katiba mpya iendelee
na kukamilika.
Waziri Wassira alitoa maelezo hayo katika mkutano wa sasa wa
Bunge la Bajeti unaoendelea mjini Dodoma, alipokuwa akijibu hoja za baadhi ya
wabunge, miongoni mwao akiwamo Halima Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe Dar es
Salaam kupitia CHADEMA.
Katika hoja zake ndani ya Bunge, Mdee ambaye naye alisusia
vikao vya Bunge la Katiba kama wenzake wengine wa UKAWA, alisema majadiliano
ndani ya Bunge la Katiba yanakiuka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba
UKAWA hawako tayari kurejea ndani ya Bunge Maalumu la Katiba Agosti, mwaka huu
endapo majadiliano hayo hayatajikita kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba.
Katika kujibu mapigo hayo na hata mapigo ya sasa ya akina
Dk. Slaa, Wassira alisema: “Kama hamrudi tutatumia kanuni zile kutafuta akidi
na Bunge litaendelea....Bunge la Katiba lipo tena lipo kisheria…. Kuna watu
wanageukageuka wanasema sheria ilivunjwa, lakini hawasemi kifungu gani
kilivunjwa,” alisema Wassira.
Wassira pia aliwahi kukaririwa akiwaambia UKAWA walisusia
Bunge la Katiba bila sababu na wanaweza kurejea katika Bunge hilo la Katiba
bila sababu.
Lakini wakati hayo yakiendelea, viongozi mbalimbali nchini
wameendelea kutoa wito kwa UKAWA kurejea katika Bunge la Katiba kuendelea na
mchakato wa kuandika Katiba mpya, kati yao ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Frederick Werema.
Werema alitoa wito kwa UKAWA kurejea bungeni huku naye akiwa
amewahi kuweka bayana kwamba hakuna haja ya kuandika Katiba mpya bali Katiba
iliyopo ya mwaka 1977 inatosha, kauli ambayo ilifanana na aliyekuwa Waziri wa
Katiba na Sheria kwa wakati huo, Celina Kombani.
Hata hivyo, kauli za viongozi hao ni kama vile zilitenguliwa
na Rais Jakaya Kikwete, ambaye alilitangazia Taifa kwamba anaanzisha rasmi
mchakato wa kuandika Katiba Mpya, tangazo ambalo lilifuatiwa na utungaji wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na tume hiyo kuanza na kukamilisha kazi yake na kisha, uundaji wa
mabaraza la Katiba kujadili rasimu ya kwanza iliyoandaliwa na Tume na kisha
Tume kuandika rasimu ya pili inayotarajiwa kuendelea kujadiliwa Agosti, mwaka
huu katika Bunge la Katiba.
Mchakato huu wa Katiba mpya hata hivyo umeshuhudia kauli
nyingine tata za viongozi, akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
William Lukuvi aliyedai Jeshi linaweza kupindua nchi endapo mfumo wa Serikali
tatu ukipitishwa, kauli aliyoitoa katika moja ya makanisa nchini alipokwenda
kumwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika shughuli za kidini.
Mbali na Lukuvi, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF)
Profesa Ibrahim Lipumba naye aliwafananisha wajumbe wa Bunge la Katiba
wanaotoka CCM kuwa ni sawa na kundi la mauaji ya kimbari nchini Rwanda,
Intarahamwe, na kisha kuondoka na wenzake ndani ya Bunge hilo katika mtindo wa
kulisusia.
__________________________________________________________________________________________