*Aondolewa chini ya
ulinzi baada Chadema, CCM kuzusha vurugu
*Ni baada ya kudaiwa
kuingiza u-CCM katika ziara ya kiserikali
KITENDO cha
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, kumkaribisha Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge, kusalimia wananchi kwenye
mkutano wa kiserikali, jana kilizua balaa na kulazimisha nguvu za dola
kuingilia kati kumnusuru mteule huyo wa Rais.
Tafrani hiyo ilizuka
jana mchana huko Goba, wakati Makalla, ambaye yupo kwenye ziara ya siku nne
kukagua miradi ya maji jijini Dar es Salaam, alipokuwa katika mkutano wa mwisho
wa hadhara kwa siku hiyo.
Kitendo cha kada wa
CCM, Madenge, kuitwa jukwaani, hakikuwapendeza wafuasi wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) waliokuwapo kwenye mkutano huo, kwa madai kuwa huo
haukuwa mkutano wa kisiasa, ndipo wanachama hao walipokumbana na wenzao wa CCM
na kuzusha vurugu kubwa zilizodumu kwa takriban dakika 30.
Wanachama wa CCM
walikuwa wakishinikiza viongozi wa Chedema; wabunge John Mnyika (Ubungo) na
Halima Mdee (Kawe) walikuwa jukwaani waondoke ili kuwe na usawa.
Vurugu na kelele za
wafuasi wa vyama hivyo ziliposhamiri, polisi walilazimika kutumia nguvu
kuwadhibiti na kuwazingira viongozi waliokuwa jukwaani kulinda usalama wao.
Baada ya kuona hali
inazidi kuwa mbaya, mwandishi wa gazeti hili alishuhudia askari polisi
wakimwondoa jukwaani Makalla chini ya ulinzi mkali na kumuingiza kwenye gari
lake, huku viongozi wa Chadema wakiendelea kuzozana na polisi waliosalia.
Akizungumza na
waandishi wa habari akiwa ndani ya gari baada ya kuondolewa jukwaani, Makalla
alisema vuruguru hizo zilisababisha wananchi kukosa haki yao ya msingi ya
kuzungumza na viongozi, kutokana na siasa kuingilia mkutano huo.
“Haya niliyataria, kwa
hiyo siwezi kushangaa. Wakati wananchi wakifurahia ujio wa Waziri katika maeneo
yao ili watoa malalamiko yao, hali imekuwa sivyo na siasa zimezidishwa, matokeo
yake tumeshindwa kuzungumza na wananchi kuhusu mambo ya msingi,” alisema.
Alisema amekamilisha
jukumu lake kwa kufika kwa wananchi kuwaeleza mipango ya Serikali katika
kutatua kero ya maji, akidai kuwa tatizo mkutano wake uliingiliwa na wanasiasa
wasio wakazi wa kata hiyo.
“Nakiri kuwa, mbali ya
wananchi kujiunganishia maji kwa njia za wizi, lakini viongozi wa Dawasco,
wanahusika kwa asilimia kubwa, kwa sababu haiwezekani watu wajiunganishie maji
kwenye bomba kubwa, ni wazi kuna msaada wa watumishi wasio waaminifu. Baada ya
ziara hii nitafumua uongozi wa Dawasco, ili tuweke watu tunaoamini tutafanya
nao kazi kama tunavyotaka sisi,” alisisitiza Makalla, wakati akizungumza na
mwandishi wa gazeti hili baadaye kwa njia ya simu.
Mbunge wa
Ubungo, Mnyika, alisema vurugu zilianzishwa na wafuasi wa CCM ambao siyo wakazi
wa eneo hilo kwa lengo la kumvuruga naibu waziri asizungumze na wananchi.
Hata hivyo, Mnyika,
ambaye mwanzoni mwa ziara hizo alipishana kauli na Makalla walipokuwa Kata ya
Mavurunza, alimtupia lawama Makalla kwa kuwaacha wananchi bila majibu
waliyokuwa wakiyasubiri kwa muda mrefu.
“Kitendo cha Makalla
kuondoka huku wanachama wake wakiendelea kufanya vurugu, ni wazi anakwepa
kujibu maswali ya wananchi kuhusu masuala ya maji, hivyo sisi hatutaondoka hadi
wanachama wetu wafahamu lini watapata maji ya uhakika,” alisema Mnyika wakati
yeye na makada wengine wa Chadema wakiendelea na mkutano ‘usio rasmi’ na
wanchama wao.
Awali, Makalla na
Mnyika, ambaye ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, walitembelea maeneo ya
Kigogo na kuwakamata wezi watano wa maji waliokuwa wakijiunganishia maji
kinyemela.
Akizungumza baada ya
kufanya ukaguzi katika nyumba hizo Makalla alisema vingozi na wananchi wana
majukumu ya kuwatambua na kuwaripoti watu ambao wanahujumu uchumi wa nchi. Watu
hao watano wamekuwa wakiikosesha DAWASCO Sh. bilioni 1.2 kwa mwezi.
Tarehe ya kuchapishwa
Imeandikwa na SHARIFA MARIRA
Hits: 36
Raia Tanzania