Maafisa nchini Ukraine wanasema kuwa ndege ya abiria
iliyoanguka nchini humo ilidunguliwa katika eneo la mashariki mwa taifa hilo
ambako waasi wanaoiunga mkono Urusi wamekuwa wakipigana na vikosi vya serikali.
Wanasema abiria wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo ya shirika la Malaysia
iliyokuwa ikisafiri kutoka Amsterdam kuelekea Kualar Lumpur wamefariki.
Wengi wa abiria hao walikuwa ni raia
wa Uholanzi.
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko
alitaja tukio hilo kama kitendo cha ugaidi.
Maafisa wa Ukraine walichapisha kile
walichotaja kuwa mawasiliano ya simu yaliyonaswa kati ya waasi wakiwaeleza
maafisa wa Urusi kwamba ni wao ndio waliohusika katika kuindungua ndege hiyo.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni
wa Ukraine, Pavlo Klimkin, amesema kuwa serikali ina ushahidi wa kutosha kwamba
ndege hiyo ilidunguliwa.
'Je waasi walihusika?'
'Tulinasa pia mawasiliano ya simu
kati ya magaidi hao wakizungumzia kundunguliwa kwa ndege hiyo.Kwa sasa
tunatafsiri sauti zao na kisha tutaziweka kwenye mtandao wa internet ili
kuthibitisha hilo."
Mabaki ya ndege ya Malaysia
iliyodunguliwa
Hata hivyo sauti hizo zilizonaswa
bado hazijathibitishwa na upande uliohuru na waasi hao wamekanusha kuhusika
wakisema kuwa ni wanajeshi wa serikali ndio walioidungua ndege hiyo