Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombale Mwiru
akizungumza katika kikao cha Bunge hilo, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin
Mjwahuzi
Kwa ufupi
Dodoma. Mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale-Mwiru amekemea
kauli za kejeli na matusi dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Akichangia mjadala wa Rasimu ya Katiba, alisema wanaombeza Warioba wanapaswa
kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa hawamtendei haki.
“Siyo sawa hata siku moja kumshambulia Warioba eti kwa sababu ya misimamo
yenu ya vyama, hata mimi japo nimestaafu lakini bado ni mwanaCCM kwa hiyo tabia
hii ni mbaya na haileti heshima,” alisema Kingunge.
Alisema kuwa misimamo ya vyama inapotokea kuwatukanisha watu tena wenye
heshima zao inakuwa ni aibu kwa chama pamoja na jamii kwa jumla na inaondoa
heshima ya mtu.
Kauli ya Kingunge imekuja zikiwa zimepita siku chache baada ya kujitokeza
kwa hali ya mashambulizi ya matusi ndani ya Bunge ambayo yalikuwa yakielekezwa
kwa Warioba kuhusu tuhuma za kuchakachua maoni ya wananchi.
Tuhuma za hivi karibuni zilitoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Tamisemi), Hawa Ghasia ambaye alimtaka Waziri Mkuu huyo wa zamani kufunga
mdomo wake kwa kuwa kazi yake imekwisha.
Mbali na huyo, Mbunge wa Mbinga Mashariki, John Komba alimfananisha Warioba
na Adam na Hawa ambao waliasi katika Bustani ya Edeni.
Akizungumzia Rasimu, mkongwe huyo alisema Katiba haitapatikana pasipokuwapo
na maridhiano na makubaliano na akawataka wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba
warudi bungeni ili waweze kujadiliana na kutengeneza katiba ya wananchi.
Kingunge aliwasifia waganga wa tiba za jadi kwa kumpendekeza kama mlezi wao
tangu 1998 ili aweze kuwawakilisha hivyo akasema hakubebwa wala kupita njia za
panya kama ambavyo wengine wanasema.
Pinda awaomba Ukawa warudi bungeni
Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana alitumia dakika 13 alizopewa na Mwenyekiti wa
Bunge la Katiba kuwaomba wajumbe wa kundi la Ukawa kurejea bungeni ili waweze
kukubaliana katika utungwaji wa katiba ya wananchi.
Pinda alisema, “Yaliyopita si ndwele, naomba nitumie nafasi hii kuwasihi
sana hawa ndugu zetu waliosusia Bunge, warudi tukubaliane pamoja katika
kutengeneza katiba ya wananchi.”