Kwa nini tukae siku 87 au 90 wakati tunajua upande wa pili
haujakamilika? Kwa mujibu wa sheria inatakiwa ridhaa ya theluthi mbili. Mwigulu
Nchemba.
Dar es Salaam/Moshi. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeanza
kumeguka baada ya baadhi ya wabunge wake ambao ni Wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba, kuunga mkono kauli ya Naibu Katibu Mkuu wake, Mwigulu Nchemba.
Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Jumanne iliyopita akichangia
wakati wa mjadala wa mabadiliko ya kanuni, alilitaka Bunge Maalumu la Katiba
lijitathmini kama lina ulazima wa kuendelea wakati hakuna uhakika wa kupatikana
kwa theluthi mbili.
Alisema kitendo cha Bunge hilo kukaa kwa siku 84 bila uhakika wa kupatikana
kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili inayohitajika kupitisha Rasimu ya
Katiba Mpya, hakiwezi kueleweka kwa Watanzania.
Nchemba alisema ni vyema kujua idadi ya wanaoshiriki awamu ya pili ya Bunge
hilo ili kutoa uthibitisho kimahesabu kama uamuzi wa kuendelea kwa Bunge
unaweza kuwa na maana.
Jana Mwigulu Nchemba alizidi kusisitiza kauli aliyoitoa akisema ni msimamo
wake binafsi kama mtoto wa maskini. Alisema anatambua jinsi walipa kodi
watakavyoumia, rasimu hiyo itakapokwama kupita kutokana na kukosekana kwa
theluthi mbili ya pande zote.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye juzi
alijibu akisema kauli ya Nchemba ni mtazamo wake binafsi na hakuongea kama
kiongozi wa chama hicho.
Lakini jana wabunge mbalimbali wa CCM walijitokeza hadharani wakisema wanaunga
mkono kauli ya Nchemba ili hesabu ijulikane badala ya kuendelea kutafuna fedha
za wananchi bila tija.
Ali Keissy
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy, alisema msimamo wa Nchemba ndiyo
msimamo sahihi ambao unapaswa kufuatwa kuliko kuendelea na Bunge wakati wakijua
kuwa theluthi mbili haitapatikana.
“Kama kuna wabunge wa CCM wanaounga mkono kauli ya Mwigulu kwa asilimia 100
basi mimi naunga mkono kwa asilimia 500 na wako wabunge wengi tu wa CCM
wanaunga mkono,” alisema.
Lembeli
Mbunge wa Kahama, James Lembeli aliliambia gazeti hili jana kuwa
alichokisema Nchemba ni ukweli ambao haupingiki.