
Hali ya
sintofahamu imeibuka katika mtaa wa Azimio, kata ya Kihonda katika manispaa ya
Morogoro, baada ya mwanamke mmoja, Veronica Madebe, kukutwa akitaka
kumtumbukiza mwanaye wa kiume ambaye ni pacha, mwenye umri wa kati ya miaka
mitano hadi saba kwenye kisima cha maji, kutokana na kinachosadikiwa kuwa ni
imani za kishirikina.
Tukio hilo
limejiri katika eneo hilo la Azimio, baada ya mwanamke huyo kukutwa na mmiliki
wa nyumba kilipo kisima hicho, Dani Haji, akijaribu kumtumbukiza kisimani mmoja
wa watoto wake pacha, kwa madai yaliyoelezwa huenda ni kupungukiwa akili, ama
ni imani za kishirikina.
Amedai
kutumwa na wakazi wawili wa eneo hilo kufanya hivyo, na wakati mwingine kudai
alikuwa kwenye kifungo na alipaswa kutoa kafara ya mtoto wake kwa kumtupa
kisimani ili afunguke baada ya kuokoka kiimani, jambo lililothibitishwa pia na
mmoja wa wajumbe wa serikali za mitaa katika eneo hilo.
Mmoja wa
familia iliyotajwa na mwanamke huyo kufanya kitendo hicho cha kikatili,
kilichozuiwa na wasamaria wema, anakiri kumfahamu mwanamke huyo lakini bila
kuwa na matatizo yeyote, na alishangazwa na hatua hiyo na alipomuona aliamua kumvaa
yeye na mtoto aliyekuwa amembeba, bila sababu zozote, hadi alipoamuliwa na
kundi la wananchi waliojitokeza.
Wananchi
wa eneo hilo walipigasimu polisi kuomba msaada wa dharura na kumpeleka mama
huyo katika ofisi za mtendaji wa kata ya Kihonda, ambako ulinzi mkali wa polisi
uliimarishwa, na baada ya muda mwanamke huyo alitolewa na kuingizwa kwenye gari
ndogo kwa nia ya kupelekwa polisi, lakini alifanya vurugu hadi polisi
walipoingilia kati na kumpakiza kwenye difenda na kuondoka naye.
Crdt: Habarika Daily