Simba imejiimarisha zaidi katika safu ya ushambuliaji.
Kiungo wa zamani wa Mlandege na Yanga, Deo Lucas amesema bado anashangazwa na klabu ya Simba kuendelea kusajili washambuliaji wakati wanajua fika wana safu mbovu ya ulinzi msimu huu.


Akizungumza na gazeti hili, Lucas alisema pamoja na Simba kufanya usajili wa maana wa mshambuliaji Dan Sserunkuma kutoka Gor Mahia ya Kenya, ni wakati sasa wa Simba kutafuta beki wa uhakika ili kuimarisha safu ya ulinzi.

Alisema huu Simba imekuwa ni moja ya timu zenye beki mbovu ambayo haijawahi kutokea, jambo ambalo limefanya wakati mwingine kufungwa mabao ya kizembe.

Lucas alisema alitarajia kuona timu hiyo inafanya usajili hasa wa beki wa upande wa kushoto, kulia na kati kwani waliopo hivi sasa hawana kiwango cha juu.

Alisema safu ya ushambuliaji haina tatizo kwani viwango vya Amisi Tambwe, Emmanuel Okwi na Elius Maguli ni vizuri hivyo ila tatizo kubwa Simba lipo katika safu ya ulinzi.

“Simba kweli wamesajili mshambuliaji wa maana huyu Sserunkuma, lakini naona bado kuna tatizo katika safu ya ulinzi. Simba wanatakiwa kuwaza kusajili mabeki ili wazuie kufungwa mabao ya kizembe kama wanayofungwa hivi sasa,” alisema Lucas.
 Cdt: Mwananchi

 
Top