Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walioko katika kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa (Monusco) cha kulinda amani nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC, wameripotiwa kuuawa.


Askari walioripotiwa kuuawa ni wawili na Pia, askari 13 wa jeshi hilo wameripotiwa kujeruhiwa na wengine wanne hawajulikani walipo.
Askari hao wanadaiwa kukumbwa na mkasa huo katika shambulio la kushtukiza lililofanywa na wanaodhaniwa kuwa waasi wa kikundi cha Allied Democratic Forces (ADF) katika eneo la Beni, lililoko katika Jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa nchi hiyo.
Shambulio hilo lilitokea wakati timu ya wanajeshi hao wa  Monusco ilipokuwa kwenye msafara wa ulinzi kwa raia kama mamlaka yao yalivyo.
Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni, mamlaka za Tanzania hazikuwa tayari kuthibitisha taarifa hizo, ingawa Umoja wa Mataifa (UN) ulizithibitisha.  
 Askari wa JWTZ wakiwa kwenye mazoezi
BAN KI-MOON
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN, na kupatikana jijini Dar es Salaam kupitia kwa Ofisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja huo (UNIC), Stella Vuzo, Katibu Mkuu wa UN Ban-Ki- Moon, alilaani vikali mauaji dhidi ya askari hao.
Kadhalika mkuu huyo wa UN alilaani unyama unaendelea kufanywa na kundi hilo dhidi ya raia maskini wasio na uwezo wa kujilinda katika eneo la Beni.
“UN inabaki imara kuchukua hatua zote stahiki kwa mujibu wa kifungu namba 2211 cha mwaka 2015 kuwalinda raia na kuyasambaratisha makundi yote yenye silaha katika eneo hilo la Mashariki mwa DRC,” alisema.
Alituma salamu za rambirambi kwa familia za askari waliopoteza maisha yao na wengine walioathirika na kwa serikali ya Tanzania.
Tukio hilo linafuatia lingine lililotokea Mei 4, mwaka huu, wakati helikopta iliyokuwa imembeba Kamanda wa Operesheni za Monusco huko DRC iliposhambuliwa na makundi yenye silaha yasiyofahamika. 
WAZIRI MWINYI
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi, alipoulizwa na NIPASHE jana, alimtaka mwandishi kuwasiliana na makao makuu ya JWTZ, akisema ndiyo wenye taarifa za kina kuhusiana na suala hilo.
“Naomba upige (simu) makao makuu ya Jeshi, wao ndio wenye details (taarifa). Hata mimi nahitaji kutoka kwao,” alisema Dk. Mwinyi.
MSEMAJI WA JWTZ
Hata hivyo, Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alipotakiwa na NIPASHE kuelezea tukio hilo, alisema kwa jana hakuwa na taarifa zozote za kuuarifu umma kuhusiana na suala hilo.
“Nipe muda nifanyie kazi, kama lipo tutaelezana,” alisema Meja Masanja.
Alisema atakuwa katika nafasi ya kuzungumzia suala hilo leo baada ya kupata taarifa kamili.
ASKARI WALIOKWISHAUAWA DRC
Hao wanakuwa maofisa wanne wa JWTZ walioko Monusco kuuawa DRC, baada ya maofisa wengine wawili kuuawa nchini humo. 
Ofisa wa kwanza wa cheo cha meja aliripotiwa kuuawa kwa bomu lililorushwa na waasi wa vuguvugu wa M 23 katika mapigano makali yaliyotokea katika mji wa Goma, Agosti 28, mwaka jana.
Meja huyo, Khatibu Shabaab Mshindo, aliuawa baada ya kujeruhiwa na bomu hilo akiwa kazini na akavuja damu nyingi wakati akikimbizwa hospitali na kusababisha kifo chake.
Wakati Mshindo aliyekuwa miongoni mwa askari wa Tanzania wanaounda Monuco akifikwa na mauti, wapiganaji wengine 10 walijeruhiwa.
Askari  mwingine wa JWTZ mwenye cheo cha luteni aliyekuwa akishiriki katika kikosi hicho aliuawa wakati wa mapigano na waasi hao. 
Iliripotiwa kuwa, askari huyo alipigwa risasi ya kichwa na kufariki papo hapo.
Habari hizo zilieleza kuwa, mbali na kuuawa kwa mwanajeshi huyo, waasi wa M23 nao wengi waliuawa na wengine wengi walijeruhiwa.
Kuuawa kwa askari huyo kulitokea siku 47 tu tangu kuuawa kwa askari saba wa Tanzania waliokuwa wakilinda amani katika Jimbo la Darfur, nchini Sudan na kikundi cha wanamgambo wa Janjaweed.
Chanzo Nipashe
 
Top