Jeshi la polisi Mkoani Simiyu Linamshikilia Chigila Gilala mkazi wa kijiji cha Bukingi Kata ya Malampaka Wilayani Maswa (45) Kwa kosa la kukutwa na Viungo vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu likiwemo Fuvu la Kichwa.

Mtuhumiwa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM katika kijiji hicho na Mganga wa tiba asili alikamatwa nyumbani kwake, baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa  alikuwa amewahifadhi majambazi kwa ajili kugangwa (kuzindikwa).
 
 Akitoa taarifa kwa waandishi wa kamanda wa  jeshi la polisi Mkoani Simiyu Gemini Mushy alieleza kuwa tukio hilo la kukamatwa kwa mwenyekiti huyo lilitokea Mei 9 mwaka huu  majira ya saa 11 jioni katika kijiji hicho.

Kamanda Mushy alisema kuwa askari wakiongozwa na mkuu wa upelelezi katika wilaya ya Maswa walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwepo kwa majambazi nyumbani kwa mganga huyo, kuwa alikuwa amewahifadhi kwa ajili ya kuwazindika.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo walifanya msako nyumbani kwa mwenyekiti huyo, ambapo  alibainisha kuwa walianza kufanya upekuzi ndani na nje ya nyumba.

“Wakati wakifanya upekuzi huo walikutana na mfuko wa sandarusi ukiwa chini ya lundo la kuni nje ya nyumba  ya mwenyekiti huyo na katika mfuko huo kulipatikana fuvu la kichwa pamoja na mifupa ya mikono au miguu vinavyodhaniwa kuwa ni viungo vya binadamu” Alisema Mushy.

Kamanda alieleza kuwa jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi kama kweli viungo hivyo ni vya binadamu na kama anahusika na uwepo wa viungo hivyo kutokana na  kukutwa nje ya nyumba yake.
 
Top