Bwana majaaliwa Kassim Majaaliwa, ambaye ameidhinishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, alizaliwa
tarehe 22 Desemba mwaka 1960 yaani miaka 55 iliyopita.
Kitaaluma ni Mwalimu aliyepata elimu yake ya Ualimu katika
chuo cha ualimu cha Mtwara mwaka 1991–1993.
Akitokea katika ukuu wa wilaya alioupata mwaka 2006 alijiunga
na bunge mwaka 2010 alipogombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ruangwa
mkoani Lindi.
Baadaye aliteuliwa kuwa naibu waziri wa tawala za mikoa na
serikali za mitaa ofisi ya waziri mkuu wakati wa serikali ya awamu ya nne.
Bw Majaliwa ameidhiniswa kuwa Waziri Mkuu baada ya jina lake
kuwasilishwa bungeni na Rais wa awamu ya tano wa Tanzania John Pombe Magufuli.
Amepigiwa kura na wabunge 258 kati ya 351 walioshiriki, ikiwa
na maana kwamba amepitishwa na asilimia 73.5 ya wabunge.
Majaliwa Kassim anatokea kusini mwa Tanzania eneo ambalo mtu
wa mwisho kutoka ukanda huo kuwa waziri mkuu alikuwa Mzee Rashid Kawawa
aliyekuwa Waziri Mkuu miaka ya mwanzoni ya uhuru.
Waziri mkuu huyu mpya anakuwa mtu wa 11 kuwa Waziri Mkuu
tangu Tanganyika ilipopata uhuru ambapo Waziri Mkuu wa Kwanza alikuwa Baba wa
Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mawaziri wakuu wawili kati
ya watangulizi wake wamehamia katika vyama vya upinzani
Jimbo la Ruangwa linapatikana Kusini Mashariki mwa Tanzania
Waziri Mkuu kwa mujibu wa
Katiba ya Tanzania atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji
wa kila siku wa kazi na shughuli za Serikali, atakuwa na madaraka ya kuongoza
shughuli za serikali Bungeni.
Atakuwa na madaraka ya kutekeleza au kusababisha utekelezaji
wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo rais ataagiza yatekelezwe.
Pia Waziri Mkuu atakuwa na madaraka ya kumshauri rais kuhusu
uteuzi wa Mawaziri.
Anayo madaraka ya kumshauri rais kuhusu uteuzi wa wakuu wa
mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri.
Waziri Mkuu huyu ni mpenzi wa mchezo wa mpira wa miguu na kwa
kipindi kilichopita alikuwa Kocha wa timu ya soka inayoundwa na wabunge.