Watu wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamewaua kwa kuwapiga risasi wafanyakazi wawili wa kiwanda cha vinywaji baridi jamii ya Coca Cola cha Bonite Bottles cha mjini Moshi na kupora mamilioni ya fedha.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, alithibitisha kutokea kwa tukio
hilo na kueleza kuwa lilitokea Aprili 20, mwaka huu saa 12:15 jioni katika
maeneo ya Soweto chini karibu na kituo cha Redio cha Kill Fm, kata ya
Soweto, wilayani Moshi.
Alisema
majambazi hayo yakiwa na silaha za moto wakitumia usafiri wa pikipiki mbili
ambazo namba zake hazijafahamika, walivamia gari aina ya Toyota Hiace
lenye namba za usajili T 803 ATR lilitoka kwenye makusanyo ya fedha za mauzo.
Kamanda
Kamwela alisema gari hilo lilikuwa likisindikizwa na mlinzi wa kampuni hiyo
akiwa na bunduki aina ya Short gun yenye namba za usajili 8710653
ikiwa na risasi tano.
“Hata
hivyo, mlinzi huyo, Edson Shamba (56), mkazi wa Matindigani aliyekuwa
anasindikiza gari hilo, aliuawa kwa kupigwa risasi maeneo ya kichwani na
kufariki dunia papo hapo na dereva, Amini Mselemu, mkazi wa mtaa wa Chunya,
alipigwa risasi maeneo ya kifuani, tumboni na mkononi alifariki
wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC,” alisema.
Alisema watu wanne waliokuwa ndani ya gari hilo ambao ni mawakala wa
mauzo wa kampuni hiyo, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro
kwa uchunguzi zaidi.
Miili
ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha KCMC.
Chanzo Nipashe