BARAZA la Ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) linatarajiwa kukutana wakati wowote hivi karibuni kwa ajili ya kujadili mwelekeo wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, imefahamika.

Baraza hilo linaundwa na waliokuwa wenyeviti na makamu wenyeviti kwa ngazi ya Taifa wa chama hicho katika miaka ya nyuma na mkutano huo utakuwa ni mara ya kwanza kufanyika tangu lilipozinduliwa rasmi miaka miwili iliyopita.

Wanaounda baraza hilo ni marais wastaafu wa Tanzania; Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Karume na Dk. Salmin Amour, Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela na Pius Msekwa.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM aliye karibu na viongozi hao aliliambia gazeti hili wiki kwamba viongozi hao watakutana kwa mara ya kwanza ili kujadili masuala muhimu ya chama hicho, likiwamo suala la nani abebe bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi ujao.

“ Hili baraza lilipoundwa hawakulazimishwa wakutane mara ngapi kwa mwaka au kwa sababu gani. Wao watakapoona ni muhimu watakutana wakati huohuo. Nimeambiwa kwamba sasa wako tayari kukutana.

“ Kwa hali ilivyo sasa ni muhimu kwao kukutana. Chama hakijatoa ratiba rasmi ya mchakato huu wa kusaka mgombea ndani ya chama na hili limesababisha matatizo mengi.

“ Kabla vikao vya chama havijaanza rasmi, ni muhimu kwa baraza kutoa mwelekeo wa nini kifanyike. Ni matarajio ya baadhi yetu kwamba ushauri huo wa baraza utakifanya chama kingie kwenye mchakato huo kikiwa kimoja na kiumalize salama,” alisema mjumbe huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Kwa mujibu wa mabadiliko yaliyofanywa na CCM mwaka 2012, baraza hilo liliundwa kwa lengo la kutoa ushauri kwa chama katika masuala mbalimbali yanayohusu chama hicho na serikali.

Kuundwa kwa baraza hilo kulisababishwa na uamuzi wa kuwafanya viongozi hao wastaafu kutoingia katika vikao vya juu vya maamuzi ya chama kama ilivyokuwa zamani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Halmashauri Kuu ya CCM wakati wa kuundwa kwa Baraza hilo, Mwinyi atakuwa ni Mwenyekiti wake na Msekwa amepewa wadhifa wa kuwa Katibu wa Baraza.

Kwa namna lilivyo sasa, baraza hilo lina idadi sawa ya wajumbe kutoka Bara na Visiwani, ambapo kila upande una wajumbe watatu.
Kinyang’anyiro cha kuwania kupitishwa na CCM kimepamba moto na sasa kuna taarifa kuwa upinzani baina ya kambi hasimu umefikia katika kiwango cha hatari.

Gazeti hili lina taarifa kwamba baadhi ya wanaotajwa kutaka kuwania nafasi hiyo hivi sasa wanapata taabu hata kunywa chai au kula chakula kwa pamoja kwa sababu za kiusalama.

Hadi sasa, CCM haijatangaza ni lini hasa wagombea wake wanataka kuwania urais wataanza kuchukua fomu kwa ajili ya kutaka kupitishwa na chama hicho; jambo ambalo limeleta hali ya mkanganyiko ndani ya chama.

Wakati baraza hilo la wazee likiundwa, yalikuwepo maneno kwamba limeundwa ili kuwaondoa wastaafu hao katika taratibu za kichama kwenye ule utaratibu uliopachikwa jina la ‘kuondoa mizengwe’.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya CCM kutangaza kuunda baraza hilo miaka mitatu iliyopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alisema baraza hilo halikuundwa kwa lengo la kuwaondoa wazee hao kwenye vikao vya chama bali kuwapa wigo mpana zaidi wa ushauri wao kuzingatiwa.

“Uundwaji wa Baraza la Ushauri la Wazee umetokana na mawazo ya wazee wenyewe wastaafu wa chama hicho ambao wamebaini ipo haja ya kuwa na chombo hicho kutokana na sababu mbalimbali.

“Jambo kubwa ambalo linapotoshwa sana ni la uamuzi wa NEC kuunda Baraza la Ushauri la Wazee. Uamuzi ambao kimsingi ulifikiwa kwenye kikao cha NEC cha mwezi Aprili mwaka 2011 mjini Dodoma kikao ambacho kiliridhia kufanyika kwa mageuzi ndani ya Chama.

“Kikao cha Februari 12, 2012 cha NEC kiliridhia tu mabadiliko ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2010 ili kuruhusu kuundwa kwa baraza hilo,” anasema Nape.

Katika maelezo yaliyowekwa na Nape kwenye tovuti ya CCM, kiongozi huyo alisema wazo la kuundwa kwa baraza hilo limetokana na ushauri wa baadhi ya wazee wenyewe wastaafu wakizingatia wingi na urefu wa vikao husika, na si mpango au mkakati wa kuwaengua makusudi wastaafu hao kama inavyodaiwa na baadhi ya wapotoshaji.

“Ilikuwa ni ushauri wao kwamba baada ya kustaafu badala ya kulazimika kuhudhuria vikao vya kitaifa kila mara basi wapewe muda wa kupumzika na wanapotakiwa kutoa ushauri watumiwe badala ya utaratibu wa sasa wa kulazimika kuhudhuria vikao ambavyo kwa kweli ni vingi na wakati mwingine huisha usiku wa manane.

“Baada ya wazo la wazee wetu kupumzika, huku tukizingatia kuwa busara zao bado ni muhimu sana kwa chama na taifa, busara ikatumika badala ya kupumzika kabisa basi tuunde Baraza la Ushauri la Viongozi wa Kitaifa wastaafu.

“Na hii haina maana kuwa hawaruhusiwi kuhudhuria vikao vya chama na kuwa hawatatumika kwa kazi za chama na taifa kwa ujumla, isipokuwa mabadiliko haya yanaondoa ulazima wa wao kuhudhuria vikao hivyo kama ilivyokuwa mwanzo.”

Nape alisema pia kwamba CCM imefanya uamuzi huo baada ya kubaini kwamba chama makini chochote kitatafuta utaratibu bora wa kuwaenzi waasisi wake na kuendelea kuvuna busara na hekima zao katika kuendelea kukijenga chama.

Alisema CCM imeonyesha mfano mzuri unaostahili kuigwa na vyama vingine na kwamba kuundwa kwa baraza hilo na kutambuliwa rasmi na katiba ya chama ni uthibitisho tosha wa namna CCM inavyothamini wastaafu hawa.

“Chama Cha Mapinduzi kinathamini sana busara na mchango wa wastaafu hawa katika ujenzi wa Chama na Taifa kwa ujumla hakiwezi kuwaong’oa au kuwatupa kama inavyojaribu kupotoshwa na baadhi ya watu. Tuwatendee haki wazee wetu hawa badala ya kutumia vibaya majina yao na uamuzi

Chanzo: Raia Mwema
 
Top