Peace Sylvester (36), mkazi wa Kijenge Juu jijini hapa amefungua madai mazito kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Arusha kwa majadala mawili, AR/RB/4404/2015 KUTISHIA KUUA KWA MANENO na AR/RB/5290/2015 KUTEKELEZA FAMILIA dhidi ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Kagera, Benson Bagonza.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda jijini hapa katikati ya wiki
iliyopita, Peace alidai Askofu Bagonza ni mzazi mwenzake kwa kuzaa naye watoto
wawili, Piana Bagonza (6) na Bariki Bagonza (3) lakini akadai amemtelekeza
hivyo kuwa na maisha magumu katika kuwalea watoto hao.
Peace alisema alianza kufahamiana na askofu huyo mwaka 2006 mjini Karagwe,
Kagera akiwa ni muumini wa kanisa hilo akimtumikia Mungu kwa kuimba kwaya ya
kanisa.
Alisema katika kuonana mara kwa mara na askofu huyo ndipo uhusiano ukaanza lakini kwa makubaliano ya kutunza siri.
“Askofu aliniambia ana mke lakini ananipenda na anataka kuwa na uhusiano na
mimi. Aliniahidi kunisaidia masuala mbalimbali iwapo nitamkubalia.“Baada ya
muda niliamua kumkubalia, tukawa na uhusiano na tulikuwa tunakutana mara kwa
mara. Ilipofika mwaka 2008 nikapata ujauzito wa mtoto wa kwanza,” alisema
Peace.
Mwanamke huyo aliendelea kudai kuwa, baada ya kupata
ujauzito, askofu huyo aliamua kumhamishia Ilemela mkoani Mwanza na
kumpangishia chumba ambapo mwaka 2009 alijifungua mtoto wa kike, Piana.
Peace aliendelea kudai:
“Mtoto wangu alipofikisha umri wa
miaka miwili, yaani mwaka 2010, askofu alinihamishia hapa Arusha na
kunipangia chumba eneo la Kijenge Juu na kunitafutia kazi kwenye Hoteli ya
Safari (New Safari Hotel). Hii hoteli inamilikiwa na KKKT.” Alisema: “Askofu
alikuwa akija hapa Kijenge kumsalimia mtoto na kumwachia matumizi mbalimbali
huku akisisitiza kutunza siri zaidi.”
“Ilipofika mwaka 2011 nilipata ujauzito mwingine wa askofu ila cha kushangaza nilipomfahamisha aliniambia hataki kusikia taarifa hizo.“Niliweka msimamo wa kutotoa ujauzito na yeye akasitisha huduma mbalimbali ikiwemo fedha za malipo ya chumba alichonipangia.
“Alianza kunipigia simu na kunitisha kuniachisha kazi aliyonitafutia
hotelini bila kupewa malipo yoyote. Alikuwa akinitumia watu mbalimbali kunitishia
maisha. “Kutoka na hali hiyo nililazimika kumtafuta kiongozi mmoja wa ngazi ya
juu kanisani na kumwambia jinsi askofu alivyonitelekeza kwa zaidi ya miaka
minne bila kunihudumia nikiwa na watoto wake wawili.
“Hata hivyo, kiongozi huyo aliniambia atalishughulikia suala langu, lakini
hadi sasa hakuna kinachoendelea na nikimkumbusha amekuwa akinijibu kwa ukali na
kunikatia simu.”
Peace alisema: “Kwa sasa naishi kwa shida na watoto. Hawaendi shule baada ya kukosa ada.”
Watoto anayedai Kutelekezwa nao
Askofu Bagonza alikiri kumtambua Peace kama mzazi mwenzake ila alisema si
kweli kama hamtumii matumizi.“Mbona fedha huwa namtumia labda ameamua
kunichafua tu. Hata juzi nimemtumia shilingi 250,000 iweje asema simhudumii?”
alisema askofu huyo na kukata simu.
Kwa upande wake, Peace alipoulizwa kuhusu kutumiwa kiasi hicho cha fedha,
alisema: “Fedha hizo nilizipokea kutoka kwa wakala wa M-Pesa baada ya
jambo hilo kulifikisha kwenye vyombo vya dola (polisi).”Taarifa zilizolifikia
gazeti hili wakati linakwenda mitamboni zilieleza kuwa mwanamke huyo ameitwa
Karagwe kwenda kuongelea suala hilo.
Chanzo: Ijumaa Wikienda