Wakati historia ikiwa imeandikwa, baada ya Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowasa, kujiunga na chama Cha Demokrasia na maendeleo (Chadema), chama hicho kimesema kiongozi huyo ameondoa kifungo kwa wanachama wa CCM ambao wamekuwa wakipata kigugumizi cha kujiunga na vyama vya upinzani.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema,
Freeman Mbowe, alisema ujio wa Lowassa Chadema ambacho ni miongoni mwa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umezua hofu na minong’ono kwa
sababu Tanzania ni taifa lililolelewa kwa misingi ya hofu.
“Chadema tunakukaribisha
Mheshimiwa Lowassa pamoja na familia yako, marafiki zako na kundi la Watanzania
wanaoitafuta haki itakayopatikana ndani ya Chadema na Ukawa kwa ujumla,”
alisema.
Mbowe alisema hofu hiyo imeanzia
ndani ya CCM na kwamba baadhi ya wana-CCM wamekuwa wakimpigia simu kumweleza
kama Chadema kitakubali Lowassa ajiunge nacho atakiharibu, lakini amekuwa
akiwaeleza kamwe hawezi kukubali Lowassa ajiunge na chama hicho.
“Wamekuwa wakinipigia simu sana
wakisema huyo Lowassa akikaribishwa kujiunga atakiharibu chama, nikajiuliza
tangu lini CCM wakaitakia mema Chadema, nikajua huu ni urafiki wa mashaka, hata
hivyo, niliwaambia over my dead body Lowassa hawezi kujiunga Chadema,” alisema.
Aliongeza kuwa hofu hiyo pia
imetawala ndani ya Chadema na kuwataka wanachama watambue hicho ni chama cha wote, lakini kama kiongozi
anatambua wajibu wa kujenga mshikamano wa Taifa na hivyo ieleweke kuwa Chadema
siyo mahakama, hivyo hakiwezi kumhukumu mtu.
“Siwezi kusema wana-CCM wala
wana-Chadema ni watakatifu, nani anaweza kusema ni mtakatifu, katika Taifa
hatuwezi kwa miaka 20 tukawa taifa la visasi,” alisema.
Mbowe alisema kumleta Lowassa
ndani ya Chadema na Ukawa haukuwa kazi rahisi kwani vimefanyika vikao usiku na
mchana na kuona wakubali ajiunge kwani hata tuhuma za ufisadi zinazotolewa
dhidi yake hazina ushahidi kwani kilichopo ndani ya CCM ni vikundi
vilivyojengwa kwa ajili ya kuchafuana na kudhalilishana.
Alisema wana-CCM wenyewe wakiwamo
wabunge wamekuwa wakilalamikia utendaji mbovu uliopo ndani ya serikali ya CCM,
lakini hawezi kusema ukweli, hivyo kwa sasa Watanzania watambue kuwa nchi yetu
inahitaji fikra na mtazamo mpya na kwa utaratibu huo hata ndani ya Ukawa
wanatofautiana, lakini bado wanaelewana na kufikia muafaka katika mambo
wanayoyajadili.
“Mimi nanayejua uchungu wa
Watanzania, nitakuwa mwendawazimu kukataa kumpokea Lowasswa kiongozi ambaye
anakubalika, mwenye ushawishi mkubwa na ifahamike hatukumkaribisha Lowassa
pekee yake hapa bali na mamilioni ya watu wanaomuunga mkono.
Alisema wana-Chadema watambue
kuwa chama cha siasa ni watu, hivyo haiwezekani yeye (Mbowe) akatae mamilioni
ya watu atakuwa mwendawazimu na kwamba anaweza kufukuzwa hata uenyekiti.
Aliongeza kuwa chama ambacho
hakiamini kwamba kuna mabadiliko siyo chama na kwamba wanachama wapya
watakaojiunga na Chadema watambue kuwa chama hicho hakiongozwi na Mbowe bali
kinaongozwa kwa kufuata katiba, kanuni na miongozo ya chama.
“Kwa katiba hii ya Chadema
mtambue kuwa hatuji kugawana vyeo, ni kuimarisha chama na kwa viongozi mliojiunga
na Chadema uzoefu wenu wa kutawala unahitajika,” alisema.
Alisema Watanzania wasihofu
mwanachama aliyeanzisha Chadema na mwanachama aliyejiunga leo, wote wana haki
sawa, hivyo viongozi wa Chadema nchi nzima wawakaribishe wageni na wasihofu
kuwa watawanyang’anya vyeo kwani ndani ya Chadema hakuna suala la kugawana
vyeo.
Mbowe alisema wapo watu ambao
viongozi wa Chadema waliwatolea lugha chafu kwani hiyo ndiyo siasa na kwa
wanachama wapya wanaotoka CCM wasisite kurusha madongo upande wa pili.
Mwenyekiti huyo alimpongeza Rais
Jakaya Kikwete katika kipindi chake cha uongozi amesaidia kuimarisha upinzani.