Mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, ametangaza kuachia wadhifa huo huku akisema sababu kuu iliyomsukuma kufanya hivyo ni kupinga wanachama wa Chama cha mapinduzi (CCM) kujiunga na umoja wa katiba ya wananchi (Ukawa)
Hata hivyo, Cuf imesema chama hicho hakitatetereka kutokana na
Profesa Lipumba kujiuzulu na badala yake kitaendelea na shughuli zake ikiwamo
kushirikiana na vyama vingine washirika wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Profesa Lipumba amesema licha ya kujiuzulu wadhifa wake huo,
hana mpango wa kujiunga na chama chochote cha siasa kama baadhi ya tetesi
zilizodai kwamba anakusudia kuhamia chama cha ACT- Wazalendo.
Aidha, amekiri kushiriki mazungumzo yote yaliyofanikisha
wanachama hao akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Hata hivyo, amesema kila akifikiria, anaona dhamira yake
inamsuta kuendelea kukalia nafasi hiyo kama Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa.
“Nimeshiriki katika vikao vingi vya Ukawa vilivyotufikisha hapa,
hata hivyo dhamira na nafsi yangu inanisuta kuwa katika maamuzi yetu ya Ukawa
tumeshindwa kuenzi na kuzingatia tunu za taifa za utu, uzalendo, uadilifu,
umoja, uwazi na uwajibikaji,” ilisema sehemu ya tamko la Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba aliyasema hayo wakati akitangaza kuachia ngazi
mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alitaja sababu ya pili ya kujiondoa katika nafasi hiyo kuwa ni
baada ya yeye kuonekana kama kikwazo cha baadhi ya mambo ndani ya Cuf.
Profesa Lipumba ambaye kwa mara ya kwanza alichaguliwa kushika
nafasi ya Uenyekiti Cuf mwaka 1999, alisema kwa sasa hana mpango wa kuhamia
chama chochote cha siasa, badala yake atabaki kuwa mwanachama wa kawaida wa Cuf
kwa kuwa kadi yake ya uanachama ameilipia hadi mwaka 2020.
Alisema katika kipindi hiki, atajikita kwenye shughuli zake za
masuala ya utafiti wa kiuchumi ili kulisaidia taifa kuondokana na umaskini.
Alisema Agosti mosi, mwaka huu, alitoa taarifa kwa Kamati ya
Utendaji inayoongozwa na Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Shariff Hamad, kuwa
angejiuzulu baada ya wenzake kukamilisha taratibu za ushirikiano ndani ya
Ukawa.
Hata hivyo, kauli ya Profesa Lipumba inapingana na alichokisema
Katibu Mkuu wake, Hamad Agosti 4, mwaka huu katika Mkutano Mkuu wa Chadema
uliompitisha Lowassa kugombea urais.
Kwenye mkutano mkuu huo, Hamad alisema hakuwa na taarifa ya
Profesa Lipumba kujiuzulu.
Mwanasiasa huyo ambaye ni mchumi aliyebobea, alisema lengo la
kuunda Ukawa, lilikuwa ni kupinga maamuzi ya Bunge la Katiba lililotaka
kuchakachua Rasimu ya Pili ya Tume ya Mabadailiko ya Katiba iliyoongozwa na
Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Hata hivyo, alisema lengo hilo limekuja kupoteza maana baada ya
Ukawa kuamua kuwapokea wanachama kutoka CCM ambao walishiriki kupitisha rasimu
hiyo mwaka jana na kuandika Katiba Mpya Inayopendekezwa.
Kwa msingi huo, Profesa Lipumba alisema hana imani na watu hao
waliojiunga na umoja huo kama wakipata ridhaa ya kuongoza nchi wataleta katiba
inayozingatia maoni ya wananchi.
Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari kuwa anakerwa na
hatua ya Ukawa ambao Cuf ni chama shiriki, kushindwa kusimamia makubaliano
yaliyounda umoja huo.
Alisema Ukawa ulianzishwa kulinda maslahi ya wananchi
yaliyoainishwa kwenye Katiba iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba, na
kwamba nafsi yake inamsuta hivi sasa kuendelea na uongozi huku waliokuwa
wanaipinga Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba wakikaribishwa kuwania uongozi wa
nchi kupitia umoja huo.
Kuhusu mvutano ndani ya chama chake, Profesa Lipumba alisema
ameamua kukaa pembeni kwa kuwa ameonekana yeye kama kikwazo cha mambo fulani
fulani ndani ya Cuf.
Hata hivyo, alikataa kuyataja huku akiahidi kuyasema siku
zijazo. Profesa Lipumba alisema amekijenga chama kwa takriban miaka 16 mpaka
sasa na katika kipindi hicho, amepata misukosuko mingi ikiwamo kupigwa na
Polisi na kuvunjwa mkono alipoongoza maandamano ya wafuasi wake pamoja na
kubambikiziwa kesi ambayo inaendelea kunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu.
MAKUBALIANO YA UKAWA
Makubaliano ya kuundwa kwa Ukawa yalisainiwa Oktoba 26, 2014
katika viwanja vya Jangwani yakiwa na ajenda saba za ushirikiano; baada ya
vyama vya Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD kuungana na kususa Mkutano wa Bunge
Maalum la Katiba.
• Kuoanisha na kuhuisha sera za vyama husika.
• Kusimamisha wagombea pamoja kwenye ngazi zote za uchaguzi
kuanzia Serikali za Mitaa hadi uchaguzi mkuu kwa ngazi za madiwani, wabunge,
wawakilishi kwa upande wa Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
• Kuweka utaratibu mzuri kwa vyama vinavyounda Ukawa
kushirikiana katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwishoni mwa
mwaka jana.
• Kushirikiana katika mchakato wa kuelimisha umma kuifahamu na
kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba inayopendekezwa.
• Kujenga ushirikiano wa dhati katika mambo na hoja zote za
kitaifa na zenye maslahi kwa Watanzania.
• Kuulinda Muungano bila kuwapo migogoro ya maslahi kama ilivyo
kwenye Katiba Inayopendekezwa.
• Kuhimiza na kusimamia ushirikiano wa pamoja kati yao, asasi na
makundi mbalimbali ya Watanzania yenye nia ya dhati ya kuulinda na kuuendeleza
Muungano usio na dalili za makundi, itikadi na maslahi binafsi.
Ukawa ilizaliwa mjini Dodoma Aprili, mwaka jana wakati wa
Mkutano wa Bunge Maalum la Katiba kutokana na muungano wa wajumbe zaidi ya 200
waliokuwa wanatetea Rasimu ya Pili iliyotolewa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba. Baada ya mvutano mkali kati ya wabunge
wa Ukawa na wale wa CCM waliokuwa wanakosoa Rasimu ya Jaji Warioba, Profesa
Lipumba alihutubia Bunge na kuhitimisha kuwa Ukawa usingeweza kuendelea
kushiriki mjadala wa Katiba kwa kuwa ni ‘dhuluma’ kwa wananchi.
Alisema mjadala uliokuwa unaendelea bungeni umekuwa na utaratibu
wa ubaguzi.
“Watu wamebaguliwa humu na viongozi wakubwa wanapiga makofi, Bunge hili
limekuwa kama Bunge la Intarahamwe. Hii ni hatari kwa nchi yetu. Wapemba,
Waarabu, Wahindi, Wakongo…tumechoka kusikiliza matusi. Tumechoka kudharau
mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi, hatuwezi kuwa sehemu ya kundi
linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania, hili hatukubali,” alisema.
Baada ya hotuba hiyo, wajumbe wote wa Ukawa walitoka nje.
Profesa Lipumba anatajwa kama miongoni mwa watu wenye ushawishi
ndani ya Cuf na aliyefanikisha kukijenga mbele ya umma.