Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana
WATU watatu wa familia moja wamefariki dunia mkoani hapa kwa kile
kinachoelezwa ni kutokana na kula nyama ya ng’ombe aliyekuwa na ugonjwa
wa kimeta. Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa
amethibitisha tukio hilo na kusema marehemu hao ni wa kijiji cha
Mwaekesabe, kata ya Kimaha wilayani Chemba.
Amewataja waliokufa kuwa ni Haji Nchalo (20) na watoto pacha, Yassir
na Yassin wenye umri wa miaka saba wote wakazi wa kijiji cha Mwaekesabe.
“Tunahisi walikula nyama yenye kimeta ila uchunguzi bado unaendelea,
ukikamilika tutatoa majibu,” alisema.
Akielezea tukio hilo, baba mzazi wa marehemu hao, Salum Nchalo ambaye
naye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma akihisiwa
kula nyama hiyo, alisema watu tisa walikula nyama hiyo, wakiwemo yeye,
mkewe na watoto wao saba na watatu kati yao ndio waliofariki.
Alisema walikula nyama hiyo Jumamosi ya Mei 28 mwaka huu aliyopewa na
jirani yake Bakari Juma mara baada ya ng’ombe wake kuumwa, hivyo kuamua
kumchinja. “Nyama nilipewa na jirani yangu Bakari Juma ambaye alikuwa
amewekeza ng’ombe kwa Iddi Kibure… Kibure alimletea ng’ombe huyo akidai
anaumwa hivyo akaamua kumchinja na nyama kutupatia,” alisema.
Aliongeza kuwa, Juma aligawa nyama kwa kaya nane kijiji hapo, lakini
akaelezea kushangazwa kuona ni familia yake pekee ndiyo iliyoathirika.
Mganga wa zamu katika wodi namba 12 ilipolazwa familia ya Nchalo, Rose
Msigwa alisema waliwapima vipimo vyote wagonjwa hao na hawakuona tatizo
lolote.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Zainabu
Chaula akizungumza kwa njia ya simu alisema kwa sasa yupo mbali na
hospitali hawezi kuzungumza chochote.