Aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka nchini Burundi, Hafsa Mossi
MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka nchini Burundi,
Hafsa Mossi, ameuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi katika mji
mkuu wa Bujumbura.
Mossi aliyewahi kuwa Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki katika
serikali ya nchi hiyo, aliuawa jana katika barabara ya Gihosha eneo la
Nyankoni.
Taarifa zilizothibitishwa na Msemaji wa Polisi wa nchi hiyo, Pierre
Nkurikiye zilisema kuwa mauaji hayo yalifanyika saa 4:00 asubuhi.
Nkurikiye alisema mbunge huyo alipigwa risasi kifuani kwenye moyo na
kukimbizwa katika Hospitali ya Jeshi ya Kamenge ambako baadaye alipoteza
maisha.
EALA ni chombo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambacho
wanachama wake ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan
Kusini, ukiwa ni umoja wa kikanda wenye ushirikiano wa kibiashara huku
ukikusudia kuwa na sarafu moja na shirikisho moja la kisiasa.
Mkazi wa eneo alikouawa Mbunge huyo, Achel Majabuka alisema kuwa
alisikia mlio wa risasi na baadaye kuona watu wawili wakiondoka katika
gari baada ya kuwatishia kwa silaha wakazi wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Bunge la Afrika Mashariki katika taarifa yake
iliyotolewa Kampala nchini Uganda, ilisema kuwa Mossi ambaye pia alikuwa
Mwenyekiti wa Wabunge wa Burundi katika EALA, alipigwa risasi katika
eneo la Mulanga Mashariki mwa Bujumbura.
Alimkariri msemaji huyo wa Polisi akieleza kuwa Mossi aliuawa karibu
na nyumbani kwake, huku Mbunge mwingine wa Burundi katika EALA, Emerence
Bucumi akithibitisha kifo hicho.
Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Daniel Kidega alilaani mauaji
hayo na kumuelezea Mossi kuwa ni mchapakazi aliyekuwa amejikita
kusimamia na kutetea utengamano wa ukanda huo.
Spika huyo ambaye yuko Uganda kwa ziara ya kikazi, ameishauri
Serikali ya Burundi kuwatia nguvuni mara moja wauaji wa Mossi ambaye pia
aliwahi kuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
“Ninatoa salamu za rambirambi kwa serikali, familia, marafiki na
wananchi wa Burundi. Ninawaomba wawe watulivu katika wakati huu mgumu na
ninaamini mamlaka husika zitafanya kazi kwa haraka kuhakikisha
waliohusika na tukio hilo la kinyama wanatiwa nguvuni mara moja,”
alisema Spika Kidega.
Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza alikielezea kifo
cha mwanasiasa huyo kuwa ni cha kudharauliwa kwa serikali yake. Naye
Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko, alisema amesikitishwa na
kifo hicho cha Mbunge huyo aliyeeleza alikuwa rafiki na dada na kuwa
jumuiya imepoteza mwakilishi aliyekuwa akifanya kazi bila kuchoka.
Mwaka jana, Mossi alitembelea wakimbizi wa Burundi nchini Rwanda na
kulia, ameuawa wakati mazungumzo kuhusu mgogoro wa Burundi yakiwa
yanaendelea kufanyika jijini Arusha.
Alikuwa na Shahada ya Uandishi wa Habari na aliwahi kufanya kazi
katika BBC na alikuwa Waziri wa Burundi wa Masuala ya Afrika Mashariki
hadi Juni 2012 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa EALA.
Pia, aliwahi Waziri wa Mawasiliano, Habari, Mahusiano na Bunge na Msemaji wa Serikali ya Burundi kuanzia mwaka 2005 hadi 2007.
Burundi, taifa katika Afrika Mashariki imekumbwa na ghasia na vifo kwa zaidi ya mwaka sasa.
Mgogoro huo wenye kuendana na umwagaji damu, umesababisha watu 1,500
kuuawa, huku ukiwahusisha wafuasi wa Rais Nkurunziza na wale wanaopinga
ushindi wake wa uchaguzi wa Julai, 2015 kwa mara ya tatu, wakidai kuwa
ulikiuka Katiba ya nchi hiyo.