Watu watano wamekufa katika ajali mbili tofauti za Magari wilayani Manyoni, ikiwemo basi la Osaka kuwagonga watu watatu kwa pamoja na lori la mafuta kuligonga gari aina ya Noah na kupinduka kisha kuli lalia juu yake na kusababisha watu wawili kufa papo hapo.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hizo Kamanda wa Polisi mkoani Singida ACP Thobias Sedoyeka amesema basi la Osaka lililokuwa likitokea Musoma na kueleke Dar es Salaam , limewagonga watu watatu na kufa papo hapo, kufuatia basi hilo kutaka kulipita lori ambalo lilikuwa limeharibika katika mlima Muhalala na kukutana uso kwa uso na Fuso ambayo ilikuwa ikitokea upande wa pili, na kusababisha Fuso hiyo kuanguka na kuligonga pia lori lilokuwa bovu ambapo marehemu hao walikuwemo.
Kamanda Sedoyeka amesema baada ya saa moja lori la mafuta ya Petroli la kampuni ya Petrol Africa lililokuwa likitokea Dar es Salaam na kuelekea Kahama liligonga gari aina ya Toyota Noah kisha kulilalia kwa juu mali ya Adam Seif wa mjini Manyoni na kusababisha vifo vya watu wawili papo hapo.
Kwa upande wao mashuhuda wa ajali hizo mbili pamoja na kutupia lawama kwa gari la zimamoto kutofika eneo la tukio ikizingatiwa gari lilosababisha ajali lilikuwa na mafuta ya Petroli walikuwa na haya ya kusema.
Wahenga wanasema kufa kufaana, kuna wengine badala ya kuokoa majeruhi walikuja na madumu na kuanza kuiba mafuta na kusahau miaka minne iliyopita lori la mafuta liligonga kichwa cha treni na kusababisha vifo vya zaidi ya watu ishirini baada ya kugombania kuiba mafuta na hatimaye kuwaka moto .