Watu wawili wamekutwa
wamefariki katika nyumba ya wageni ya Kings Rest House iliyopo Mtaa wa
Bumila, Gongo la Mboto jijini Dar huku miili yao ikiwa imeungua moto.
Mmiliki wa gesti hiyo, Damian
Mng’ong’o alisema alifuatwa kanisani jana saa 1.30 asubuhi na kuambiwa
kuna chumba kimoja katika gesti yake kinafuka moshi na aliondoka
kanisani kuelekea ilipo nyumba hiyo.
Alisema alipofika aliona moshi bado unafuka huku nje kukiwa na umati mkubwa wa watu wakishangaa.
“Tulifanya uamuzi wa kufungua
mlango lakini hatukuona mtu yeyote chumbani, ndipo mmoja wa wafanyakazi
alipofungua mlango wa choo ndani ya chumba tukakuta maiti mbili zikiwa
zimechomwa. “
Alisema mhudumu wa gesti alitueleza
kuwa jana (juzi) saa tano asubuhi alikuja mwanamume mmoja akachukua
chumba na baadaye jioni alikuja kijana mwingine wakawa wameingia wote
katika chumba hicho.
“Baada ya muda nilipiga simu polisi
kuripoti tukio hilo nao waliwasili ndani ya muda mfupi wakafanya
uchunguzi wao na kuhoji baadhi ya watu, baadaye wakawaleta madaktari
kupima, kisha wakaondoka na maiti hizo mbili kwenda Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa ajili ya hatua nyingine.”
Mfanyakazi wa jikoni katika gesti hiyo
ambaye hakupenda jina lake litajwe alisema watu hao waliofariki ni
wafanyabiashara wanaouza ng’ombe katika mnada wa Pugu na mara nyingi
wakija Dar es Salaam hufikia hapo.
“Wengi wanaofanya biashara ya
ng’ombe wakija hufikia hapa, mpaka sasa sijajua kilichotokea kwa hawa
waliokufa, lakini tukio hili limewashtua wenzao kwani baadhi walipoona
tukio hili wameingiwa na hofu na kuondoka,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum
Hamduni alisema wanaendelea kuchunguza na taarifa za awali
hazijathibitisha kama waliuawa hapo gesti au sehemu nyingine na
kupelekwa hapo.
“Kuna viashiria kuwa huenda
waliuawa wakaletwa pale kwani wana alama ya kamba katika shingo kama
vile kuna mtu aliwanyonga na katika matumbo yao kuna majeraha kama
wamechomwa kitu chenye ncha kali,” alisema na kuongeza:
“Mpaka sasa uchunguzi unaendelea na
Jeshi la Polisi linafanya kazi yake na tunasubiri taarifa kutoka kwa
wataalamu wa masuala ya uchunguzi na alama za vidole ambayo itaeleza kwa
nini wao waungue lakini nguo zao zisiungue. Pia kitanda na vitu vingine
visiungue na kwa nini watu waende kuzima moto, wakati watu
wameshafariki,” alisema Hamduni.
Hamduni alisema mmoja wa waliofariki alijiandikisha kama Lameck Ludovick, mfanyabiashara na mkazi wa Dar es Salaam.