Timu ya waokozi kutoka mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na wananchi wamefanikiwa kuopoa miili ya wanafunzi wawili wa shule ya sekondari Mwika wilaya ya Moshi na sekondari ya Serengeti mkoani Mara waliozama maji kwa siku tatu wakati wakiogelea katika ziwa Chala liliopo katika wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Kamada wa polisi mkoa wa Kilimanjaro SACP Wilbrod Mutafungwa amethibitisha kuopolewa kwa miili hiyo iliyozama tangu Decemba 26 wakati wanafunzi hao walipoenda kusheherekea sikukuu ya pili ya krismas kwa kuogelea.
Amewataja waliofariki kuwa ni Mogeri Chacha mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Mwika na Julius Moranga mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Serengeti na kwamba miili hiyo imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Rombo huruma kwa uchunguzi.
Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kilimanjaro imetembelea ziwa hilo ikiongozwa na mkuu wa mkoa Bw.Said Meck Sadiki ambapo amewataka wageni wanaofika katika ziwa hilo lenye kina kirefu kuchukua tahadhari kabla ya kuruhusiwa kuogelea kwa kuwa matukio ya watu kupoteza maisha katika ziwa hilo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara.
Naye baba mzazi wa wanafunzi hao waliozama maji ambaye ni afisa wa taasisi ya kupambana na rushwa mkoa wa Kilimanjaro TAKUKURU Bw. Julius Chacha amesema juhudi za kuokoa miili hiyo siku ya tukio ilishindikana.