DAR ES SALAAM: Majonzi yametanda
kwa familia ya mtoto Gerald (2) ambaye amekutwa amekufa katika shimo
la choo cha kanisa linalomilikiwa na mwimba Injili, Boniface Mwaitege,
Kipunguni, Ukonga jijini hapa.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo
lilijiri Julai 24, mwaka huu katika kanisa hilo ambalo linakua kwa kasi
ambapo awali, mtoto huyo alifika kanisani hapo akiongozana na mama
yake.
Inasemekana kuwa baada ya kufika, mama
yake aliingia kanisani kwa ajili ya ibada na kumwacha mtoto wake huyo
nje ya kanisa akicheza na wenzake.
“Mara baada ya kumaliza ibada jioni,
mama huyo alipotoka nje hakumuona mwanaye lakini hakushtuka akijua kuwa
alirudi nyumbani. Alipofika nyumbani hakumkuta, ndipo juhudi za
kumtafuta zikaanzia hapo,” alisema shuhuda mmoja.
Akaongeza: “Baada ya juhudi za kumtafuta
mtoto huyo kushindikana ndipo wazazi wakatoa ripoti polisi huku waumini
wa kanisa hilo wakiendelea na maombi ili mtoto huyo apatikane.
“Siku ya tatu ya kumtafuta mtoto huyo
kwa maombi mazito, mwili wake ulipatikana katika shimo la choo cha
kanisa ambacho hakijaanza kutumika. Kusema kweli maombi ya waumini
naamini yalisaidia na Mungu alituonesha alivyo mwema kwa wanaomwomba.”
Uwazi lilipomtafuta Mwaitege kuhusu
tukio hilo, alisema: “Ni kweli tukio hilo lilitokea lakini Mungu ni
mwema, mwili wa mtoto ulipatikana na ulipelekwa Morogoro.”
Mwili wa mtoto huyo ulisafirishwa Julai
27, mwaka huu kwenda Ifakara, Morogoro kwa mazishi. Mungu ailaze pema
peponi, roho yake. Amina.
Chanzo: Uwazi