BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema wale wote walioomba mkopo mwaka huu na kukidhi vigezo watapewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema hayo juzi
mjini hapa wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti kwa watu watano
waliorejesha mkopo wa elimu ya juu kwa mkupuo na kwa hiari.
Badru alisema idadi ya walioomba mkopo mwaka huu ni wanafunzi 88,000
ambao bodi itahakikisha wale wote waliokidhi vigezo, wanapatiwa fedha
kwa ajili ya elimu ya juu.
Mkurugenzi huyo ambaye amehimiza walionufaika na mikopo kulipa madeni
yao, alisema mwaka jana, wanafunzi waliokopeshwa ni 55,000.
Kuhusu waliopewa vyeti ikiwa ni hatua ya kuwatambua, ni pamoja na
mfanyakazi wa VETA Shinyanga, Richard Jafu aliyerejesha kwa mkupuo Sh
14,749,950 na Francis Mwilafi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo
aliyelipa Sh 15,115,200.
Wengine ni Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga aliyerejesha Sh 255,000;
Profesa Peter Msoffe ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma
(UDOM) aliyerejesha Sh 1,430,749.
Mwingine ni Mbunge wa Biharamulo, Oscar Mukasa ambaye kiasi
alichorejesha hakikutajwa ingawa mkurugenzi mtendaji wa HESLB, alisema
amerejesha kiasi kikubwa kwa mkupuo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao walisisitiza umuhimu wa
wanufaika wa mikopo kuirejesha kwa hiari ili kuiwezesha bodi hiyo
kukopesha wanafunzi wengine.
Mbunge wa Biharamulo, Mukasa alishauri bodi hiyo kuangalia uwezekano
wa kurekebisha vigezo kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi watokao maeneo
ya pembezoni kunufaika na mikopo hiyo ya elimu. Kwa upande wake, Mbunge
wa Vwawa, Hasunga alisisitiza wabunge wanaodaiwa warejeshe mkopo kwa
mkupuo.