MHASIBU wa shule ya sekondari ya Mtakatifu Joseph, Elizabeth Asenga
(40), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
akikabiliwa na mashitaka ya kumkashifu Rais John Magufuli kwenye mtandao
wa WhatsApp.
Elizabeth alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na
Wakili wa Serikali, Leonard Chalo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma
Shaidi.
Wakili Chalo alidai kuwa, Agosti 6, mwaka huu, huku akijua Elizabeth
alituma ujumbe wenye mazingira ya kumkashifu Rais Magufuli kwa njia ya
WhatsApp kwenye kundi la kijamii liitwalo STJ Staff Social Group.
Inadaiwa aliandika ujumbe unaosema:
“Goodmorning humu, hakuna rais kilaza kama huyu wetu duniani, angalia
anavyompa Lissu umashuhuri, fala lile, picha yake ukiiweka ofisini ni
nuksi tupu, ukiamka asubuhi, ukikutana na picha yake kwanza, siku
inakuwa mkosi mwanzo mwisho”.
Baada ya mshitakiwa kusomewa mashitaka, alikana kutenda kosa hilo na
upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na
kuomba kesi hiyo iahirishwe hadi tarehe nyingine.
Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa
na wadhamini wawili, wanaotakiwa kusaini dhamana ya Sh milioni mbili.
Kesi itatajwa tena Septemba 22, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, mfanyabiashara Juma Shaban (31) amefikishwa
mahakamani hapo akikabiliwa na mashitaka sita likiwemo la kutakatisha
dola za Marekani 340,000, sawa na Sh milioni 680.
Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson, alidai mbele ya Hakimu Mkazi
Mkuu, Emmilius Mchauru kuwa, Mei 31, 2003, Dar es Salaam, kwa nia ya
kudanganya alighushi hati ya forodha akidai anasafirisha madini aina ya
dhahabu kwa Igor Davydakin.
Aidha anadaiwa kughushi hati nyingine na stakabadhi kwa nia hiyo, pia
alighushi hati ya kusafirisha mizigo akionesha kwamba ndege ya Qatar
ilikuwa inasafirisha na kupeleka madini hayo kwa Davydakin.
Esterzia alidai kati ya Aprili 20 na Mei 10, 2013 jijini Dar es
Salaam, kwa nia ya kudanganya mshitakiwa huyo alijipatia kiasi hicho cha
fedha kutoka kwa Davydakin kwa madai atampelekea madini hayo huku
akijua si kweli.
Inadaiwa, mshitakiwa alijihusisha na utakatishaji wa fedha, kwa
kuelekeza fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti ya Monteblanc Godmine
Company iliyopo benki ya Stanbic, na baadaye kuzitoa huku akijua fedha
hizo ni mazao ya kosa la kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande kwa kuwa mashitaka
ya utakatishaji fedha hayana dhamana. Kesi itatajwa tena Septemba 15,
mwaka huu.