MAMA mzazi wa mtoto wa miezi minane na mganga wa kienyeji
wanashikiliwa na Polisi kwa kuhusika na mauaji ya mtoto huyo
aliyetambulika kwa jina la Rukia Joshua kwa lengo la kujipatia utajiri.
Imeelezwa kuwa mtoto huyo aliuawa kisha kutupwa katika tundu la choo
cha Shule ya Msingi Chanela, katika kijiji cha Nassa, wilayani ya
Busega, mkoani Simiyu.
Mama na mganga huyo wanashikiliwa katika kituo cha Polisi cha wilaya ya Busega kilichoko mjini Nyashimo.
Wakihojiwa na waandishi wa habari na wakazi wa kijiji hicho, mama
huyo aliyetambulika kwa jina la Rusia Iluja alisema kuwa mganga wa jadi,
Hewa Maduhu alimuua mtoto wake ili apate moja ya vichanganyio ambavyo
vitatumika katika dawa mbalimbali ili vimpatie dawa ya utajiri.
Akisimulia zaidi Iluja aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Maduhu
aliingia ndani ya nyumba alipokuwa amelala saa 7 usiku, siku mbili kabla
ya mwaka mpya na kumwingilia kimwili bila ridhaa yake huku akitishia
kumuua kwa dawa alizonazo.
Wakati wa vitendo vyake hivyo vya kijahili, Iluja alisema Maduhu
alimwambia ya kuwa mtoto wake ana mali kubwa katika mwili wake hivyo
lazima amuue ili aweze kufanikiwa katika mambo yake.
Baada ya kusema na kumaliza ubazazi wake majira ya saa 9 usiku Maduhu
alimchukua mtoto huyo na kwenda naye kwake huku akimwamuru asitoke nje
na akitoka, atamfanyia kitu kibaya ambacho hajawahi kukifanya.
“Saa 10 alfajiri alikuja kuniambia eti Rukia amefariki na anaenda kumtupa na kunitaka nikae ndani tu atanikuta.
Alimchukua mke wake na kuelekea maeneo ya shule ya msingi Chanela
huku nikiwafuata kwa nyuma bila ya wao kuniona mpaka walipomtumbukiza
katika tundu la choo mtoto wangu,” alisema Iluja.
Alisema kuwa alikwenda katika kijiji cha Shigala ambacho anaishi
mzazi mwenzake na kueleza mambo yote aliyofanyiwa na Maduhu na hivyo
alimpeleka katika kituo cha Polisi Busega kutoa maelezo yake.
Katika mahojiano hayo, Maduhu alisema kuwa yeye kazi zake ni
kuhakikisha anawasaidia wagonjwa ili wapone lakini anashangazwa na jambo
hili la kuambiwa amemtupa mtoto chooni wakati mtoto huyo alipelekwa
kwake kupata tiba.
“Ilikuwa ni kama siku 10 zilizopita nikiwa nyumbani kwangu nilipata
wageni watatu ambao ni mama na watoto wawili huku mtoto mmoja ambaye ni
Joshua mwenye umri wa miaka minne akiwa ni mgonjwa asiyejitambua
nikaanza kumpatia dawa na kurejea katika hali yake huku mtoto mwingine
(marehemu) naye akiwa anaumwa ila si sana,” alisema Maduhu.
Aliongeza kuwa alifanikiwa kurejesha hali za watoto hao na kuwa katika hali zao za kawaida za kila siku.
Aidha aliendelea kueleza kuwa siku moja baba wa mtoto alikwenda
nyumbani kwake ili kulipa deni la tiba kwa mtoto wake lakini alipofika
alidai kuwa kwa sasa hali yake si nzuri kipesa hivyo alimuomba ampe muda
ili alipe deni hilo na alimkubalia kwa vile alikuwa anamfahamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea na utakapokamilika
watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.
Chanzo: Habari Leo