POLISI wilayani Igunga, mkoani Tabora limewakamata watu watatu wakiwa
na noti bandia za Sh 10,000 zipatazo mia nane sawa na Sh milioni nane
wakiwa wamezihifadhi kwenye ‘buti’ ya gari yao ndogo.
Waliokamatwa ni Luneka Magasha (35) mkazi wa Igunga, Zengo Magasha
(25) mkazi wa mkoa wa Lindi na James Hangalu mkazi wa Dar es Salaam.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema watu hao walikamatwa
Januari 3 mwaka huu majira ya saa sita mchana katika maeneo yaliyoko
jirani na katikati ya benki ya NMB na hoteli ya Cathay wilayani hapa.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Igunga Magharibi walikokamatwa watu
hao Luzwiro Kitano ameishukuru Polisi Igunga kwa kazi nzuri
waliyoifanya kwa kuwa fedha hizo zingeleta madhara makubwa katika uchumi
wa mji wa Igunga.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara na wazee wa mji wa Igunga
wamemuomba mkuu wa jeshi la polisi nchini Ernest Mangu kuwazawadia
baadhi ya askari waliofanikiwa kuwanasa watu hao wakiwa na fedha hizo
bandia kwa kuwa wameonesha utendaji mzuri wa kazi yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamisi Selemani alithibitisha
kukamatwa kwa watu hao ambapo alisema polisi walipata taarifa za kuwepo
kwa watu hao na baada ya taarifa hiyo walikwenda eneo la tukio ambapo
waliwakuta watu hao wakiwa na gari ndogo yenye namba za usajili T 964
BEC.
Aidha kamanda Seleman alifafanua kuwa baada ya kuwapekua kwenye gari
yao walikuta kwenye buti sh milioni nane noti za shilingi elfu kumi.
Kamanda huyo aliongeza kuwa baada ya kuwahoji watu hao walikiri kuwa
fedha hizo ni za bandia na ni mali yao na walikuwa wamejipanga
kuzisambaza katika minada ya ng’ombe ya Igunga na Ibologelo inayofanyika
siku ya jumamosi na jumatatu kwa wiki.
Hata hivyo, alifafanua kuwa fedha hizo zote pamoja na gari waliyokuwa
nayo vimehifadhiwa kituo cha polisi wilayani Igunga na ametoa mwito kwa
wananchi kuwa makini katika biashara zao kwenye magulio yao mbalimbali
hapa mkoani Tabora kwa ujumla.
Chanzo: HABARILEO