“Vipimo vinatolewa bure kwa wagonjwa wote wanaokuja kupima
hospitalini hapa na tunawaomba wananchi, anayejisikia ana dalili za ugonjwa huu
aje mara moja,” .PICHA|MAKTABA
Kwa ufupi
Ni katika Hospitali ya Amana, wasema asiyelazwa anadaiwa
Sh30,000. Mganga Mfawidhi atoa maelezo.
Dar es Salaam. Licha ya Serikali kutangaza kuwa matibabu ya
homa ya dengue ni bure, inadaiwa kuwa baadhi ya watoa huduma katika Hospitali
ya Amana wamekuwa wakiwatoza wagonjwa Sh30,000 huku wengine wakitakiwa kulazwa
kabla ya kupimwa na baadhi wakiambiwa vifaa vimekwisha.
Hayo yanadaiwa kutokea wakati Kaimu Mganga Mfawidhi wa
Hospitali hiyo, Dk Gilbert Ngua alinukuliwa Mei 16, mwaka huu akisema hakuna
tatizo hilo kwani ilikwishapokea vipimo 100 vya ugonjwa huo vilivyokuwa
vimetumika ni 44 na kusisitiza kwamba wagonjwa wanapimwa bure.
“Vipimo vinatolewa bure kwa wagonjwa wote wanaokuja kupima
hospitalini hapa na tunawaomba wananchi, anayejisikia ana dalili za ugonjwa huu
aje mara moja,” alisema Dk Ngua.
Hata hivyo, mmoja wa wagonjwa, Sarah Mwendapole alisema jana
kuwa mmoja wa watoa huduma kitengo cha maabara aliwatangazia kuwa vifaa hivyo
vimewaishia huku wengine wakielezwa kuwa utaratibu uliopo ni kwamba wanatakiwa
walazwe ili vipimo vyao vichukuliwe wakiwa wodini.
“Nimeandikiwa niende maabara nikapime kipimo cha dengue
lakini nilipofika nimeelezwa kuwa nitoe Sh30,000 lakini baada ya kuona hiyo
hela sina ndipo wakaniambia vifaa vimeisha halafu kuna utaratibu anayeandikiwa
kipimo hicho aende akalazwe vipimo vitatolewa akiwa wodini,” alisema Mwendapole.
Mgonjwa mwingine, Abdallah Sayuni alisema aliandikiwa kipimo
hicho Jumamosi lakini alitakiwa akalazwe na kipimo kitachukuliwa akiwa wodini.
Akizungumzia madai hayo, mhudumu mmoja wa maabara ambaye
hakutaka kutaja jina lake alisema mgonjwa anayeandikiwa kipimo cha dengue
lazima alazwe na vipimo vyao vitachukuliwa wakiwa wodini.
“Mgonjwa anayeandikiwa kipimo cha Dengue lazima akalazwe
halafu vipimo vyao vitachukuliwa wakiwa wodini huo ndiyo utaratibu uliopo
sasa,” alisema.
Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa na Dk Ngua ambaye alisema
wahudumu wanaowataka wagonjwa waliokwenda kupima dengue walazwe kabla ya
kuchukuliwa vipimo vyao, ni kosa na analifanyia kazi suala hilo.
“Mgonjwa anayelazwa kabla ya kupima ni yule mwenye dalili
zote za ugonjwa huo na amezidiwa. Analazwa huku vipimo vyake vikichukuliwa
akiwa wodini si kwa wagonjwa wote,” alisema Dk Ngua.
Alisema tangu Ijumaa hadi jana, wagonjwa wapya waliopokewa
katika hospitali hiyo walikuwa 44, kati ya hao, 22 waligundulika kuwa na
dengue, sita walilazwa na wengine waliruhusiwa kurudi nyumbani.