Kesi hiyo imewashangaza wanaharakati wa haki za kibinaadamu ambao wamesema kuwa msichana aliyeozwa kwa mume anayemzidi umri zaidi ya mara mbili yake anafaa kuchukuliwa kama mwathiriwa na wala siyo muhalifu



Bi harusi wa miaka 14 nchini Nigeria ameshtakiwa kwa kuwaua watu wanne akiwemo mumewe wa miaka 35 baada ya kuweka sumu ya panya katika chakula alichoandaa kwa sherehe za harusi yake.


Kesi hiyo imewashangaza wanaharakati wa haki za kibinaadamu ambao wamesema kuwa msichana aliyeozwa kwa mume anayemzidi umri zaidi ya mara mbili yake anafaa kuchukuliwa kama mwathiriwa na wala siyo muhalifu


Msichana huyo aliyetambulika kwa jina la Wasila Tasiu kutoka familia maskini katika eneo lenye idadi kubwa ya Waislamu huenda akakabaliwa na adhabu ya kifo Shahidi wa kwanza wa kiongozi wa mashtaka Lamido Abba Sorron-Dinka alikuwa msichana wa miaka 7 anayejulikana kama Hamziyya ambaye alikuwa akiishi katika nyumba moja na Tasi’u pamoja na mumewe Umar Sani wakati bi harusi huyo alipoweka sumu ya panya katika chakula hicho.


Akizungumzia zaidi kuhusu kisa hicho ambacho kimevuta hisia za wengi msichana huyo wa miaka 7 alisema kwamba Tasi’u alimpa fedha ili kununua sumu ya panya kutoka duka moja liliko jirani kwa maelezo kuwa alitaka kukabiliana na panya waliokuwa wakimsumbua nyumbani kwake.


‘’Aliniambia niende dukani kununua dawa kuwadhibiti panya waliokuwa wakimsumbua mara kwa mara katika chumba chake,’’ Hamziyya aliiambia mahakama. Upande wa mashtaka baadaye ulisema kuwa badala yake Tas’u aliweka sumu hiyo ya panya katika chakula ambacho alikuwa amekiandaa kwa sherehe baada ya harusi kwa kuwa alijuta uamuzi wake kuolewa na Sani.


Ushahidi wa Hamziyya uliungwa mkono na Abuwa Yussuf muuzaji duka katika mji wa Unguwar Yansoro ambaye alithibitisha kuuza sumu hiyo kwa mtoto huyo.


Jirani ya Sani mwenye umri wa miaka 30 ambaye ni mkulima Abdulrahim Ibrahim alitoa ushahidi ambapo alisema kwamba alipewa chakula hicho kilichopikwa na Tasiu.’’ Nilipoletewa chakula hicho niliona vipandevipande vyeusi’ ‘aliiambia mahakama.


Alikula vipande vinne vya matonge vilivyotengezwa na maharagwe lakini hakupendelea ladha yake’’, alisema na kuongezea kuwa ni Umar pekee aliyeendelea kula. Baadaye alisema kuwa alimuona bwana harusi Sani katika bustani akiwa mgonjwa na akamua kuchukua uamuzi wa kumpeleka nyumbani.

Alisema kuwa wakati akiendelea kumhudumia bwana harusi huyo alipata taarifa kuwa watu wengine watatu ambao walikuwa wamekula chakula hicho walifariki dunia ghafla. Viongozi wa mashtaka walidai kwamba chakula cha Tasiu kilichowekwa sumu kiliwaua watu wanne .


Nigeria haijawahi kumyonga mtoto aliyefanya uhalifu tangu mwaka 1997ambapo taifa hilo liliongozwa na dikteta Sani Abacha. Lakini kesi inayomkabili msichana huyo inafuatiliwa kwa karibu na mashirika ya haki za binadamu.


Bibi harusi huyo ambaye hakuwa tayari kuzungumza lolote wakati alipopandishwa mahakamani amesema kuwa hakufurahishwa na hatua ya kuolewa na Sani. Awali alisema kuwa familia yake ilimlazimisha kuolewa na mtu ambaye hakuwa na mapenzi naye hivyo ingekuwa jambo la hatari kuendelea kudumu katika ndoa hiyo.


Ndoa hiyo iliyofungwa wiki moja iliyopita katika kijiji cha bwana harusi cha Ungwar Yansoro kilichoko umbali wa kilimeta 100 kutoka mji wa Kano. Nigeria inatajwa kuwa moja ya nchi zilizoko katika eneo la Magharibi mwa Afrika zinazoandamwa na matukio mengi ya ndoa za utotoni.


Nyingi ya ndoa hizo zimekuwa zikifanyika katika eneo la Kaskazini lenye idadi kubwa ya jamii ya Kiislamu ambao wengi wao wanaelezwa kuwa ni maskini. Mwaka uliopita Nigeria ilitikisa katika vyombo vya habari baada msichana wa miaka minane kukacha kuolewa katika dakika za mwisho. 

 
Top