
Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Said Mkasiwa alitoa hukumu hiyo mwishoni
mwa wiki na kusema kuwa mshtakiwa ambaye ni mkazi wa Majohe, atatumikia
kifungo hicho baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na
mashahidi watano dhidi yake.
Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemhukumu kifungo cha maisha
mfanyakazi wa ndani, Habibu Adamu (20) baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka
mtoto wa miaka sita na kumsababishia maumivu.
Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Said Mkasiwa alitoa hukumu hiyo mwishoni mwa
wiki na kusema kuwa mshtakiwa ambaye ni mkazi wa Majohe, atatumikia kifungo
hicho baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi watano
dhidi yake.
“Mshtakiwa atatumikia kifungo cha maisha ili iwe fundisho kwa vijana na
wanaume wenye tabia za kikatili kama hizi dhidi ya watoto,” alisema na kuongeza
kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi akiwamo daktari ndiyo
uliomtia hatiani.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mahakama ilimpa nafasi mshtakiwa kujitetea.
Katika utetezi wake, alisema anaumwa vidonda vya tumbo, hivyo anaiomba
Mahakama imhurumie kwa kupunguzie adhabu.
“Hakimu naomba Mahakama yako inipunguzie adhabu, nina vidonda vya tumbo,”
alidai mshtakiwa.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi hayo na kumhukumu kifungo
cha maisha jela.
Awali, Wakili wa Serikali, Silvia Mitanto aliiomba Mahakama hiyo kutoa
adhabu kali dhidi ya mshtakiwa kutokana na kuongezeka kwa kwa vitendo vya
ubakaji dhidi ya watoto wadogo.
Mitanto alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 2013 katika eneo
la Majohe Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Chanzo: Mwananchi