Mechi kama hiyo ilipofanyika
mwaka jana, 2013, Yanga ilifungwa magoli 3-1 na kusababisha aliyekuwa kocha
wake Ernie Brandts kutimuliwa pamoja na benchi lake la ufundi. Mwaka huu ni
zamu ya kocha Marcio Maximo kufungashiwa virago vyake baada ya kunyukwa mabao
2-0 katika mechi ya Mtani Jembe iliyofanyika Jumamosi iliyopita katika Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam, na huu ukiwa ni mchezo wa nane wa ushindani
baada ya michezo saba tu ya ligi kuu ya Vodacom ya nchi hiyo.
KOCHA Maximo ambaye
alipokelewa kwa vifijo na nderemo na mashabiki na wanachama wa Yanga mwezi Juni
mwaka huu baada ya kutangazwa kuwa kocha mpya wa timu yao, amewaaga rasmi wachezaji
wa timu hiyo kwenye mazoezi uwanja wa Sekondari ya Loyola ya jijini Dar es
Salaam.
Mazoezi hayo ya Jumanne
asubuhi yaligeuka simanzi baada ya Maximo kuwakusanya wachezaji wake na
kuwambia kuwa kuanzia hiyo jana hakuwa kocha wa timu hiyo tena na kuwatakia
maisha mema ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wachezaji wa klabu hiyo walielezea kutoridhishwa na uamuzi wa uongozi
wa klabu hiyo kumuacha kocha wao na mshambuliaji Hamis Kiiza kutoka Uganda.
Mmoja wa wachezaji hao alisema
"Ni kweli kocha ametuaga asubuhi daa! ndio hivyo tumesikitika lakini
hatuna jinsi."
Naye mchezaji mwingine ambaye
hakutaka jina lake litajwe alisema "Inaumiza sana jana (juzi) tumefanya
nae mazoezi vizuri kabisa tena amechangamka kama kawaida kumbe nyuma kuna mambo
yanaendelea, leo asubuhi tumeenda mazoezi kama kawaida tukijua tunafanya mazoezi
matokeo yake anasema acheni kila kitu kaeni hapo nataka kuzungumza na
nyinyi".
Mchezaji mwingine wa timu
hiyo alisema "Hakuna mchezaji kwa kweli aliyependezwa na kitendo cha
uongozi, yaani kwenye mazoezi asubuhi ilikuwa kama msiba, 'mood' ya kufanya
mazoezi iilisha kabisa, yaani hakuna aliyekuwa na hamu ya kuendelea na mazoezi.
"Tumefanya kidogo
mazoezi tukaondoka, ukiangalia ni sawa tumefungwa cha muhimu ilikuwa ni kukaa
chini na kuzungumza na kuangalia cha kufanya, kama kuna mapungufu basi
yafanyiwe kazi, mimi sijaona haja ya kumfukuza kocha hasa kipindi kama
hichi."
Meneja wa timu hiyo Hafidhi
Saleh alikiri Maximo kuwaaga wachezaji kabla ya mazoezi ya timu hiyo kwanza
akiwapa moyo wajitume kwa kuwa ni wachezaji wazuri na timu ni nzuri na kuwataka
kuongeza bidii ili wafike mbali.
"Kwa kweli inasikitisha
hakuna mchezaji wala mtu aliyefurahia, kama yupo labda kimoyomoyo ila dah
imetuumiza, ni mazoea cha muhimu tugange yajayo hayo mengine tuwaachie
viongozi."alisema Saleh
Mchezo wa Mtani Jembe ambao
ni wa kujifurahisha na kuongeza utani kati ya timu hizo, umegeuka kuwa kipimo
cha ubora wa kocha hata kama kocha huyo anafanya vizuri katika michezo ya ligi
kuu. Hadi wakati anafukuzwa, kocha wa Yanga Mbrazil Marcio Maximo, timu yake
inashika nafasi ya pili baada ya Mtibwa inayoongoza katika msimamo wa ligi hiyo
kutokana na michezo saba tu iliyochezwa.
Baadhi ya mashabiki wameunga
mkono uamuzi wa kumtimua Maximo wakisema timu haikuwa na uwezo wa kupambana na
timu pinzani, huku wengine wakipinga uamuzi huo kuwa haukustahili kuhukumu
uwezo wa kocha huyo katika mchezo mmoja wa kirafiki na kusahau nafasi
inayoshikiliwa na timu katika msimamo wa ligi kuu.
Crdt: BBC
Crdt: BBC