Vuguvugu la Watangaza nia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchukua na kuwania nafasi ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu linazidi kuwa kubwa kila kukicha.
Idadi ya makada wa chama hicho wanaowania nafasi
hiyo, inazidi kuongezeka ambapo mpaka sasa, zaidi ya makada 40 wamejitokeza
kwenye makao makuu ya chama hicho, Dodoma na kuchukua fomu za kuwania nafasi
hiyo.
Licha ya utitiri huo wa wagombea, mtu anayetakiwa
ni mmoja tu na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, ndivyo wanavyozidi
kuibuka watu wanaobadili kabisa upepo wa kisiasa ndani ya chama hicho, wengine
wakipewa nafasi kubwa huku wengine wakionekana kuwa ‘mamluki’ katika safari
hiyo ya kuelekea Ikulu .
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai Lowassa, ni
kada ambaye mpaka sasa, nguvu zake za ushawishi miongoni mwa wananchi na
wanachama wa chama hicho zimejipambanua pengine kuliko mgombea mwingine yeyote,
huku akipewa nafasi kubwa ya kurithi kiti kitakachoachwa wazi na swahiba wake
wa siku nyingi, Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Hata hivyo, licha ya dalili zote za awali
kuonesha kwamba Lowassa ana nafasi kubwa ya kuteuliwa na chama hicho, hasa
kutokana na jinsi anavyokubalika miongoni mwa wananchi, akifunga mitaa kila
anapokwenda kuomba udhamini mikoani, duru za kisiasa ndani ya chama hicho,
zinaonesha kwamba uwezekano wa mbunge huyo wa Monduli kupenya ni mgumu kutokana
na sababu kadha wa kadha.
Kwa mujibu wa Profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam ambaye alizungumza kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini,
mfumo usio rasmi utakaotumiwa na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kuwachuja
wagombea hao ili kumpata mmoja atakayekiwakilisha chama, unaonesha ‘kutokuwa
rafiki’ kwa Lowassa.
MFUMO UTAKAOTUMIKA
“Unajua chama tawala kinatumia mfumo wa ‘X, 5, 3,
1’, yaani maana yake ni kwamba watajitokeza watangaza nia wengi ambao idadi yao
haina kikomo (X) ambao sekretarieti kuu ya chama itayapitia majina yote kisha
kuyapeleka kwenye Kamati Kuu (CC) ambayo itayachuja majina hayo kwa kuzingatia
vigezo 13 vilivyowekwa na chama ili kupata majina ya wagombea watano
watakaopelekwa kwenye Halmashauri Kuu.
“Majina hayo matano yatachujwa na Halmashauri Kuu
ili kupata majina matatu ambayo yatapelekwa kwenye mkutano mkuu wa chama utakaopitisha
jina moja kwa hiyo kanuni ya ‘X, 5, 3, 1’ itakuwa imetimia,” alisema profesa
huyo.
UGUMU UNAANZIA HAPA
Profesa huyo aliliambia Uwazi Mizengwe
kwamba ugumu kwa Lowassa kupenya kwenye mchujo huo, unatokana na sababu
zifuatazo:
“Unajua hiki ninachowaambia siyo rasmi lakini
ndiyo utaratibu utakaotumika na kama hamuamini mtajionea wenyewe. Katika majina
matano yatakayopitishwa na Kamati Kuu, uwezekano mkubwa ni kwamba chama
kitazingatia mambo kadhaa.
“La kwanza ni suala la
Muungano,
ili kuulinda muungano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, lazima nafasi mbili
kati ya tano za watakaopitishwa, zitatoka kwa wagombea wa Zanzibar ambapo mpaka
sasa, uwezekano mkubwa unaonesha Makamu wa Rais, Mohamed Ghalib Bilal na Jaji
Mstaafu, Augustino Ramadhan ndiyo wanaopewa nafasi.
“Pili chama kitazingatia suala la jinsia ambapo
lazima katika nafasi hizo tano, moja itaenda kwa mwanamke. Habari za chini kwa
chini zinaonesha Dk. Asha Rose Migiro ndiye mwenye nafasi kubwa ya kupita kwa
kigezo cha jinsia, kwa hiyo katika zile nafasi tano, zinakuwa zimesalia nafasi
mbili.
“Waziri mkuu ndiye mtendaji mkuu wa serikali, kwa
lugha nyingine lazima awe ni mtu anayekubalika ndani ya chama kabla ya kupewa
wadhifa huo mkubwa wa kumsaidia rais. Mizengo Pinda amekuwa waziri mkuu wa
kipindi kirefu katika utawala wa Rais Kikwete tangu Lowassa alipojiuzulu.
“Kwa kuwa naye amechukua fomu, haitakuwa rahisi
kwa wajumbe wa kamati Kuu ‘kumchinjia baharini’. Haipo rasmi lakini uwezekano
mkubwa ni kwamba anaweza kubebwa na wadhifa wake ingawa suala la upendeleo
ndani ya chama huwa halipewi kipaumbele.
“Kama ikitokea hivyo, maana yake, tayari kutakuwa
na majina manne; Bilal, Jaji Augustino, Dk. Migiro na Pinda. Katika ile hesabu
ya majina matano yanayotakiwa, inabakia nafasi ya mtu mmoja tu ambayo ndiyo
hiyo itakayogombaniwa na akina Lowassa, Membe, Dk.Magufuli, Profesa Mwandosya,
Wasira, Makamba na makada wengine wote waliosalia. Unafikiri itakuwa rahisi kwa
Lowassa kupenya?” alisema profesa huyo.
UPEPO WA KISIASA ULIVYO
Licha ya ufafanuzi huo jadidi kutoka kwa mtaalamu
huyo wa siasa, Uwazi Mizengwe lilienda mbele zaidi na kupima upepo wa
kisiasa ulivyo miongoni mwa watangaza nia. Katika uchunguzi huo uliofanywa na
gazeti hili, imebainika kwamba mpaka sasa hakuna mtangaza nia ambaye amekuwa gumzo
kama ilivyo kwa Lowassa.
“Jamaa anakubalika sana, tuacheni utani. Yaani
tangu siku ya kwanza alipotangaza nia pale Arusha, sote tuliona jinsi
alivyokusanya umati mkubwa wa watu ambao haujawahi kutokea na hakuna mtangaza
nia mwingine aliyevunja rekodi hiyo.
“Yote tisa, kumi ni ziara za mikoani kusaka
wadhamini zinazofanywa na Lowassa. Yaani kila mkoa anaokanyaga, anapokelewa na
maelfu ya wananchi na wanachama wa chama hicho. Maeneo yote aliyopita ameacha
gumzo. Hiyo ni ishara kwamba Lowassa anakubalika sana,” alisema Profesa huyo,
mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Kama CCM wataamua kufumba macho na kutozingatia
kigezo cha kukubalika, basi wanaweza kulikata jina la Lowassa lakini kama
wataangalia mgombea anayeuzika kama Rais Kikwete alivyosema kwenye maadhimisho
ya miaka 37 ya CCM kule Songea, ipo wazi kwamba Lowassa atapenya kwenye hatua
zote za mchujo,” Ismail Mabula, mtaalamu wa siasa kutoka taasisi moja isiyo ya
kiserikali iitwayo Free Political Forum, yenye makao makuu yake jijini Dar es
Salaam aliliambia Uwazi Mizengwe.
CCM WANASEMAJE?
Uwazi Mizengwe halikuishia hapo,
liliwatafuta viongozi wa CCM na kutaka kujua wanazungumziaje mchakato huo.
Kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya chama hicho (jina limehifadhiwa) alipoulizwa
kuhusu mchakato wa mchujo utakavyokuwa, alisema sifa na vigezo anavyotakiwa
kuwa navyo mgombea vipo wazi na kwamba chama hicho kitasimamia kwa umakini
utaratibu na kanuni.
Alisema CCM haitachuja wagombea nje ya kanuni na
kwamba mgombea asiyekuwa na vigezo hatabakizwa kwa sababu ya cheo chake, hasa
viongozi wa serikali kwani ni wadogo kuliko viongozi wa chama.
“Suala la kuteuliwa kutoka Kamati Kuu kwenda
Halmashauri Kuu haliangalii vyeo, ukisema Waziri Mkuu na Makamu wa Rais
wataingia kwa vyeo vyao utakosea kwa sababu kichama hao ni watu wadogo, kama
utakumbuka katika uchaguzi wa mwaka 2005, John Malecela alikuwa Makamu
Mwenyekiti wa chama lakini jina lake lilikatwa mapema.
“Vigezo 13 wanavyotakiwa kuwa navyo wagombea vipo
wazi, tunasubiri muda tu ili tuanze kazi ya kuwachuja wagombea kumpata mmoja
anayestahili kupeperusha bendera ya chama,” alisema ofisa huyo mwandamizi wa
chama.
Kwa mujibu wa ratiba, mchakato wa kuchukua fomu
utafikia mwisho Julai 2, mwaka huu kisha vitafuata vikao mbalimbali vya
uchujaji wa majina ya wagombea kwa kuanza na kikao cha Kamati ya Usalama na
Maadili, Julai 8.
Kikao hicho kitafuatiwa na kikao cha Kamati Kuu
(CC), Julai 9 kisha Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai
12 na 13, mwaka huu ambapo hapo ndipo jina la mgombea mmoja atakayechaguliwa
litakapotangazwa