Kamanda wa polisi mkoani Tanga Frasser Kashai
Baadhi ya wakazi wa Handeni mkoani Tanga wameandamana
kulaani mauaji yaliyofanywa na watu wasiojulikana baada ya kuvunja nyumba moja
na kupora mali, kisha kumuua kijana aliyekuwa ndani ya nyumba hiyo.
Watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wamevunja
nyumba na kupora mali mbalimbali kisha kumnyonga mwanafunzi Isihaka Beda wa
darasa la saba shule ya msingi Jitegemee iliyopo makao makuu ya wilaya ya
Handeni hatua ambayo imesababisha majonzi makubwa kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Maandamano na vilio vya wakazi wa wilaya ya
Handeni kufuatia watu wasiojulikana kuvunja nyumba ya mkazi mmoja Abida Zubeir
wa eneo la Kivesa lililopo makao makuu ya wilaya ya Handeni ambapo wanadaiwa
kuvunja na kuiba TV, Deki, Godoro na vifaa vingine mbalimbali kisha kumnyonga
mwanafunzi beda kwa kutumia mti wa kitanda cha miti wakati alipokuwa akipiga
mayoe.
Kufuatia hatua hiyo baadhi ya makundi ya
wazee na viongozi wa mitaa wa wilaya ya Handeni wameiomba serikali kuhakikisha
wanawatumia baadhi ya vijana kusaidiana kufichua wahalifu ambao wanaishi nao
katika jamii ili kupunguza kasi ya vitendo vya mauaji ya kutisha yanayotishia
usalama wa wananchi.
Kamanda wa polisi mkoani Tanga naibu kamishna
wa jeshi la polisi Frasser Kashai amethibitisha kutokea kwa tukio na amewaomba
wananchi wa wilaya ya Handeni na mkoa wa Tanga kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa
jeshi la polisi ili kuhakikisha kuwa vitendo hivyo vinakomeshwa.
CRDT: Ngara Yetu