SIMULIZI YA KUSISIMUA Sehemu ya Nane
Ilipoishia
“Pumbavu. Unanifanya
mimi mjinga sio?” Mama Suzy alifoka.
Kule chini ya uvungu
hali ya Ayubu ilizidi kuwa mbaya. Alianza kujuta uamuzi wake aliouchukua wa
kumkubalia Suzy. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakimuenda mbio huku kijasho
chembamba kikimtoka. Alibana mdomo wake ili kuzuia pumzi zisitoke kwa sauti.
Endelea……
“Umeanza lini kuvaa nguo za kiume?” mama Suzy alihoji swali ambalo lilipelekea
kushusha pumzi kwa Suzy na Ayubu kule chini ya kitanda.
“Samahani mama. Sitarudia tena”
“Usifanye ujinga mwanagu si unajua kuwa nakupenda” Mama Suzy alisema kwa upole.
“Ndio mama” alijibu Suzy kwa upole. Mama Suzy alitaka kuondoka lakini alipofika
mlangoni alirudi tena.
“Kuna mkebe ulikuwa huku chini ya uvungu” alisema mama Suzy huku akitaka
kuinama kuchungulia chini ya mvungu. Suzy alimuwahi na kuinama yeye.
“Ngoja nikusaidie mama” alisema Suzy na kuinama. Lakini alitafuta kile kimkebe
bila ya mafanikio. Alimkonyeza Ayubu na kumwambia atulie kimya. Suzy
alipokikosa kile kimkebe alitoka.
“Mama sijakiona”
“Basi ngoja nikiangalie mwenyewe” alisema mama Suzy akitaka kuinama.
“Nimekumbuka mama”
“Nini?”
“Nilifanya usafi na kukipeleka stoo” Suzy aliongopa.
“Haya nenda ukanitafutie” Alisema mama Suzy huku akiondoka. Mama Suzy
al;ipotoka Suzy alijibwaga kitandani na kupumua kwa nguvu. Hakuamini kama mama
yake ametoka pasipo kugundua kitu kilichokuwa kikiendelea. Ayubu alimgusa Suzy
mguuni ili kujua kilichokuwa kikiendelea. Suzy aliinuka na kuelekea mlangoni na
kuchungulia nje. Alipoona hapakuwepo na mtu alimpa Ayubu ishara ya kutoka.
Ayubu alifanikiwa kuingia chumbani kwake bila kuonekana. Hakuweza kuamini kama
amepona kutoka kwenye mdomo wa mamba.
****
Maisha ya Ayubu na Suzy
yalibadilika na kuwa kama vile mtu na mpenzi wake. Wazazi wao walipokuwepo
waliitana kaka na dada. Lakini walipobaki wenyewe waliitana majina kama vile
Sweety , babe, Honey, Darling, na mengine kadha wa kadha ya kimapenzi. Kila
walipopata nafasi waliutumia muda wao kiufasaha. Mapenzi kati yao yalizidi
kunawiri huku watu wakiamini kuwa wawili wale walikuwa ni ndugu walioshibana.
Baada ya miezi mitatu tangu walipoanza mchezo wao Suzy alianza kubadilika.
Alionekana akinawiri, huku matiti yakiongezeka ukubwa. Alikuwa na kila dalili
ya kuwa na ujauzito. Alipojigundua kuwa amenasa alimfahamisha haraka Ayubu.
“Ayubu”
“Niambie mpenzi”
“Nina tatizo”
“Tatizo gani? Ayubu alihoji kwa mashaka. Kitu kilichomshangaza ni kwamba Suzy
alikuwa akilia badala ya kuzungumza.
“Sasa kama unalia mi ntakusaidiaje?”
“Nina…nina…nina ujauzito Ayubu” alisema na kuanza kulia kwa sauti.
“Mungu wangu!! Una….una mimba! Nimekwisha” Ayubu alihamaki huku ameweka mikono
kichwani. Alionekana kuchanganyikiwa asijue cha kufanya. Taswira ya matatizo
aliyokumbana nayo punde alipoingia jijini ilimjia tena. Tatizo lililomkuta
safari ile akaliona ni kubwa zaidi, alifahamu kuwa uhai wake ulikuwa matatizoni
endapo Mzee Manyama angeligundua lile. Aliinua macho na kumtazama Suzy usoni.
“Suzy, baba yako ataniua”
“No! sitakutaja”
“Kweli Suzy?”
“Nakupenda sana Ayubu, siwezi kukutaja”
“Nashukuru sana Suzy. Hata mimi nakupenda” alisema Ayubu na kumkumbatia Suzy.
Pamoja na kwamba Suzy
alimuahidi kuto kumtaja kwa baba yake, lakini Ayubu moyo wake ulipoteza amani
kabisa. alikuwa akiwaza na kuwazua kitu ambacho kingetokea endapo baba yake
Suzy angegundua suala lile. Kuna wakati alipata wazo la kutoroka lakini ahadi
aliyopewa na Suzy ya kuto kumtaja ilimpa moyo wa kuvumilia.
Siku zilivyozidi kwenda Suzy naye ndivyo alivyozidi kubadilika. Hatimaye wazazi
wake waligundua hali ile. Mama Suzy alimuita mwanawe kwa urafiki na kumuuliza
mtu aliyehusika na ujauzito ule lakini Suzy alionekana kuwa mgumu kumtaja.
Baada ya sauti ya upole kushindikana ilibidi ukali utumike. Mama Suzy alifoka
huku akimtandika makofi binti yake kumlazimisha amtaje mhusika wa lile tukio.
Kelele za mama Suzy zilimgutusha Ayubu ambaye alikuwa chumbani kwake
amepumzika. Ilimbidi kutoka na kusimama mlangoni kwa Suzy kusikiliza
kilichokuwa kikiendelea. Alipogundua kuwa alikuwa akiadhibiwa kwa kugoma
kumtaja mtu aliyempa ujauzito, Ayubu alirudi chumbani kwake na kujiweka tayari
kwa matokeo yoyote.
Wakati mama Suzy alipokuwa akimfokea mtoto wake mzee Manyama alikuwa anarejea
kutoka kazini. Alisimama pale mlangoni kusikiliza muelekeo wa mazungumzo yale.
Alipogundua kuwa lilikuwa suala la binti yake kupewa ujauzito alifungua mlango
na kuingia bila kubisha hodi. Walipomuona wote wawili walishituka, mama Suzy
akajibaraguza ili mume wake asigundue.
“Kuna nini?”
“Hakuna kitu mume wangu”
“Pumbavu, unafuga maradhi? Nimesikia kila kitu” alisema Mzee
Manyama huku ameshika kiuno. Alimtazama Suzy kwa hasira na kujikuta akipumua
kwa nguvu.
“Sikiliza we mbwa, Tusipotezeane muda. Sema ni nani aliyefanya huo
upuuzi?” mzee Manyama alitoa amri. Alikuwa hapendi kubishiwa alipotaka ufanye
kitu fulani. Mama Suzy aliinuka na kwenda chumbani kwa Ayubu na kupaza sauti
kumuita. Ayubu moyo ulimpasuka akahisi amekwisha kutajwa. Alipotoka mama
Suzy alimtuma mtaa wa pili kuchukuwa pesa zake alizokuwa akizidai kwa mama
Halima. Lengo la mama Suzy ni kumfanya Ayubu asijue kilichokuwa kikiendelea.
Ayubu alipokuwa akielekea kwa mama Halima alikuwa ametingwa na
mawazo. Alifahamu kuwa kurudi kwa mama Suzy ndio ulikuwa mwisho wa maisha yake.
Alimfahamu mzee Manyama kuwa alikuwa tayari kupoteza uhai wa mtu kwaajili ya
binti yake.
Mama Halima alimpatia Ayubu kiasi cha shilingi Elfu hamsini. Ayubu
alianza safari ya kurudi nyumbani kwao. Alipokaribia alisimama na kutafakari
cha kufanya. Alipokumbuka ahadi ya Suzy alipata nguvu ya kwenda lakini
alipowaza endapo Suzy angemtaja ingekuwaje, hapo nguvu zilimuishia kabisa.
Alikwenda moja kwa moja hadi nyuma ya nyumba na kujibanza
akisikiliza kilichokuwa kikiendelea chumbani kwa Suzy. Alimsikia Suzy akilia
huku akikataa kumtaja mtu aliyempa ujauzito. Mzee Manyama alipoona Suzy alikuwa
akionesha kiburi, alikwenda chumbani kwake na kurudi na bastola. Alimnyooshea
Suzy huku akiwa na hasira.
“Heri kuishi bila mtoto kuliko kuishi na mbwa kama wewe. Ayubu
anatosha kuwa mtotowetu. Sasa chagua moja kati ya kufa ama kumtaja mtu
aliyekupa huo ujauzito”
“Basi….basi….baba…nam…namtaja”
“Mtaje Suzy, utakufa mwanangu” mama Suzy alisihi.
“Ni…ni….ni..A..A…Ayubu”
“What?” Mzee Manyama alihamaki kusikia kuwa Ayubu ndiye mhusika wa
ujauzito ule. Kule nje Ayubu moyo ulimpasuka baada ya kusikia jina lake
limetajwa. Mama Suzy na mume wake hawakuamini kama kijana waliye muamini na
kumpenda angeweza kuwalipa kwa kuwafanyia vile.
“Shukurani ya punda ni mateke. Lazima afe!” alisema Mzee Manyama na
kufungua mlango kutoka kwa hasira kwenda kummaliza kijana aliyeharimu maisha ya
binti yake.
Itaendelea....
