
“Hivi inaingilia akilini kweli kwa mfanyakazi TRL
unasimamisha treni na kuiba mafuta? Ninadhani haingiii akilini hiki ndicho
walichokifanya baadhi ya niliowafukuza wenzenu.” Dk Mwakyembe
Dar es
Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewafukuza
kazi wafanyakazi sita wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) na kuamuru wakamatwe na
polisi kwa tuhuma za kuhujumu shirika hilo.
Mbali na uamuzi huo, pia Dk Mwakyembe ameigiza Bodi ya TRL kuanzia jana
kusitisha mkataba na Kampuni ya Translog inayojihusisha na upakuaji na kuhesabu
mizigo katika treni, badala yake kazi hiyo ifanywe na wafanyakazi wa shirika
hilo.
Akizungumza jana katika mkutano na wafanyakazi, Dk Mwakyembe alisema kuwa
wizara yake haiwezi kuvumilia hujuma na wizi unaofanywa na watumishi wachache
wasio waaminifu.
“Kila siku nimekuwa napambana Waziri wa Fedha Saada Mkuya ili awaongezee
mishahara, lakini nakutana na hivi vituko vya wizi kutoka kwa baadhi ya
wafanyakazi wenzenu,” alisema Dk Mwakyembe.
“Nina ushaidi wa video jinsi baadhi yao walivyohusika na jambo hili,
nimechoka kupiga siasa na wakishakamatwa nataka uchunguzi wa mali zao uanze
mara moja na ikiwezekana zipigwe mnada,” alisema.
Aliongeza: “Kibaya zaidi, kuna wafanyakazi ambao kazi kubwa ilikuwa
kukatisha tiketi kwa abiria kwa Sh61,200, lakini cha ajabu kiasi kinachoingia
TRL ni Sh16,000 huu si wizi.”
Kuhusu Translog Dk Mwakyembe, aliigiza Bodi ya TRL kusitisha mkataba huo
alilodai unainufaisha kampuni na shirika hilo likishindwa kupiga hatua za
maendeleo kama miaka ilivyopita.
“Shirika lenyewe bado linajikongoja, halafu bodi bado mnang’ang’ania
kufanya kazi na kampuni hii. Kuanzia leo, sitaki kuona fedha yoyote inayotoka
TRL kuwalipa Translog na atakayefanya hivyo tutamkata kwenye mshahara wake,”
alisema Dk mwakyembe.
Katika hatua nyingine, Dk Mwakyembe amemwagiza katibu mkuu wizara hiyo,
Shaaban Mwinjaka kuungana na timu ya watu wanne ya wataalamu kutoka idara
mbalimbali, ikiwamo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchunguza mabehewa
mapya matatu yaliyoanguka hivi karibuni na jana mkoani mkoani Morogoro.
Awali, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (Trawu) John Kiwele alisema
hatua hiyo ya waziri ya kuwafukuza kazi watumishi wasiowaaminifu ni nzuri
na alitaka uchunguzi wa kina ufanyike katika ununuzi wa mabehewa ambayo alidai
kuna harufu ya rushwa ndani yake.
Kutoka Mwananchi