Wanafunzi waliokuwa kwenye maandamano ya kudai fedha zao za
kujikimu walidai kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wenzao waligongwa na gari ya
polisi iliyokuwa ikitawanya maandamano hayo ambayo polisi waliyaita ni haramu
na kufariki dunia.
Kufuatia uvumi ulioenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii na katika mji
wa Dodoma na viunga vyake kuwa kuna wanafunzi waliofariki dunia kufuatia
maandamano yaliyofanyika juzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Nassor Mzee amesema kuwa
taarifa hizo si za kweli.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mjini hapa, Dk Mzee
amesema kuwa hakuna maiti yoyote ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma
iliyopokelewa katika hospitali hiyo na kusisitiza kuwa taarifa hizo siyo za
kweli.
“Hapa hospitalini hakuna maiti yoyote ya mwanafunzi wa Udom na hata baada ya
kupata taarifa hizo nilikwenda mapokezi kwa ajili ya kupata taarifa na kwenye
wodi zote hapa hospitalini lakini hakuna mwanafunzi hata mmoja wa kutoka Udom
aliyefika hapa kutibiwa,” amesema Dk Mzee.
Aliongeza kuwa, “Hata kwenye chumba cha kuhifadhia maiti hakuna maiti yoyote
ya mwanafunzi wa udom… labda kama waliamua kwenda kuzihifadhi maiti hizo kwenye
hospitali nyingine nje ya hapa lakini hapa hakuna maiti yoyote kutoka Udom.”
Awali baadhi ya wanafunzi waliokuwa kwenye maandamano ya kudai fedha zao za
kujikimu walidai kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wenzao waligongwa na gari ya
polisi iliyokuwa ikitawanya maandamano hayo ambayo polisi waliyaita ni haramu
na kufariki dunia.
Pia katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa juzi na jeshi la
polisi haikutaja vifo wala majeruhi zaidi ya kutaja idadi ya wanafunzi
waliotiwa mbaroni kufuatia maandamano hayo kuwa ni 84.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema kuwa wanafunzi
wote waliokamatwa katika maandamano hayo wameshafikishwa mahakamani
kujibu mashtaka yanayowakabili ya kuvuruga amani chuoni na kufanya
maandamano haramu.