“Kila mmoja kachafuliwa kwa kuzushiwa kashfa ama kwa baadhi ya watangaza nia wenzao au wapambe wao jambo ambalo ni hatari,” alisema.
Dar es Salaam. Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutoka vyuo vikuu, wamekitaka chama hicho kuchukua hatua za makusudi kutokana na kuanza kushamiri kwa taarifa za watu kuchafuana kupitia mitandao ya kijamii.

Mwenyekiti wa umoja huo, Gaston Onyango alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi kuwa kuna taarifa mbalimbali zinasambazwa za kuwachafua baadhi ya makada wa chama hicho zinazopaswa kutolewa ufafanuzi na viongozi wa ngazi ya juu badala ya kuzikalia kimya.

“Hatutaki kusema wala kumlenga mtu, lakini kama CCM itaendelea kufumbia macho vitendo vya kuchafuana kupitia mitandao ya kijamii kwa wana-CCM waliojitokeza kutangaza nia ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, hali itakuwa tete ndani ya chama,” alisema Onyango.

Alisema karibu makada wote waliojitokeza hadharani na kutangaza nia ya kuwania kiti hicho wamekuwa wakichafuliwa siku hadi siku kwa kuzushiwa kashfa mbalimbali.

“Kila mmoja kachafuliwa kwa kuzushiwa kashfa ama kwa baadhi ya watangaza nia wenzao au wapambe wao jambo ambalo ni hatari,” alisema.

Naye Gabrieli Munasa mwanachama wa UVCCM, alisema taarifa mbalimbali zinazoendelea kusambazwa zikihusisha kashfa za ufisadi zinalenga kukiyumbisha chama.

Alisema kuna wanaCCM wamejiandaa kuchafuana kwa maslahi binafsi na siyo ya chama wala Taifa.

“Lazima watu hawa tuwasake na tuwatambue na ikibidi tuutangazie umma kuwa hawafai katika jamii.

“Kuna watu wanahangaika usiku na mchana na wanatumia fedha nyingi kuwachafua wenzao wakishirikiana na wapambe wao. Sisi kama vijana wa CCM katu hatuwezi kuikubali hali hii,” alisema Munasa.

Alisema misimamo ya watu hao hailengi kuwachafua wapinzani wao tu, bali na chama na Serikali.
 
Top