Kwa upande wa wakili wa Serikali, Mohammed Salum, aliiomba
mahakama kulitupilia mbali ombi hilo kwa madai kuwa hakuna madhara ama upungufu
katika shtaka hilo na siyo lazima kila kifungu kitajwe.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Januari 15, mwaka huu, itatoa uamuzi katika kesi inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chadema, Halima Mdee (35) na wenzake wanane wa kufuta shtaka la pili linalowakabili washtakiwa hao ama la.
Uamuzi huo ulipaswa kutolewa jana na Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda
uliahirishwa.
Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka ya kutotii amri halali ya Jeshi la
Polisi ya kufanya mkusanyiko usio halali. Wakili anayewatetea, Peter Kibatala
aliiomba mahakama kulifuta shtaka hilo la pili katika kesi hiyo kwa madai kuwa
lina upungufu wa kisheria.
Shtaka linaloombwa kufutwa ni la kufanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la
kutembea kwenda kwenye Ofisi ya Rais kinyume na kifungu cha 74 na 75 cha Sheria
ya Kanuni ya Adhabu, sura ya 16.
Kwa upande wa wakili wa Serikali, Mohammed Salum, aliiomba mahakama
kulitupilia mbali ombi hilo kwa madai kuwa hakuna madhara ama upungufu katika
shtaka hilo na siyo lazima kila kifungu kitajwe.
Awali, washtakiwa hao walipokuwa wakisomewa maelezo yao ya awali mahakamani
hapo, waliyakubali kuwa ni maelezo yao binafsi na kuyakana mashtaka yote
yanayowakabili mahakamani hapo.
Washtakiwa wengine ni pamoja na Rose Moshi, Renina Peter, Anna Linjewile,
Mwanne Kassim, Sophia Fangel, Edward Julius, Martha Mtiko na Beatu Mmari. Kwa
pamoja wanadaiwa kuwa Oktoba 4, 2014, katika Mtaa wa Ufipa, bila kuwa na
uhalali walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi,
Emmanuel Tillf kwa niaba ya Jeshi la Polisi.
Ilidaiwa kuwa, washitakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha
124 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
Chanzo: Mwananchi