Mbowe pia alitoa nyaraka nyingine zinazoonyesha jinsi Nec
imekuwa ikiandaa kwa siri utaratibu wa BVR bila kuwashirikisha wadau.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe, amedai kuibua nyaraka zinazoonyesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(Nec), ilishauriwa na mtaalamu wa mashine za BVR kutoka Marekani kuwa Tanzania
haijawa tayari kwa teknolojia hiyo.
Akifungua kikao cha baraza la uongozi wa chama hicho Kanda
za Nyanda za Juu Kusini jana alisema, Mshauri Mwelekezi kutoka Marekani Darell
Geusz ambaye ni mtaalam wa mashine za usajili wa wapiga kura kutumia mfumo wa
kieletroniki (BVR) alichukuliwa kuishauri Tume kuhusu mashine hizo.
Alisema nyaraka hizo zinaonyesha ushauri uliotolewa na
mtaalam huyo kwa Tume ni kuwa Tanzania haijawa tayari kwa teknolojia hiyo kwa
sababu hakuna vifaa, utaalam na
wataalam.
“Mtaalamu huyo alishauri wakilazimisha kuendelea kuzitumia
mashine hizo watasababisha machafuko ya kisiasa nchini,” alisema.
Mbowe pia alitoa nyaraka nyingine zinazoonyesha jinsi Nec
imekuwa ikiandaa kwa siri utaratibu wa BVR bila kuwashirikisha wadau.
Wakati Mbowe akiibua madai hayo, Naibu Katibu Mkuu wa chama
hicho (Tanzania Bara), John Mnyika, alisema kauli ya Jaji Mstaafu Damian Lubuva
dhidi ya viongozi wa siasa aliyoitoa
juzi imelenga kufunika kombe mwanaharamu apite.
Juzi Jaji Lubuva aliwaasa viongozi wa siasa kutotumia
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kama mwanya wa kuanzisha fujo.
Mnyika alisema Chadema hakitanyamaza bali kitaendelea kutaka
upungufu katika mashine za BVR kufanyiwa kazi.
Alisema chama chake kimenasa taarifa za mawasiliano kati ya
Tume na Taasisi ijulikanayo kama, IPSITI zikionyesha kwamba Nec haijafanya
marekebisho ya mapungufu yaliyopo kwenye BVR.
Alisema serikali hususan Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
anapaswa kujitokeza hadharani kuelezea sababu za kutoshughulikia upungufu ulio
onekana licha ya ripoti ya wataalam kubainisha.
Pia alisema Pinda anapaswa kuueleza umma sababu za serikali
kutotoa fedha kamili kwa Tume hiyo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa ni
pamoja na kutoa elimu kwa wapiga kura.
“Pinda awaeleze Watanzania ukweli kuwa Serikali haina fedha
kwa sababu wahisani walisitisha misaada ya kibajeti, hii ilitokana na kashfa za
ufisadi wa kifedha,” alisema na kuongeza:
“Wahisani walisitisha fedha za misaada ya kibajeti kabla ya
bunge halijafikia maamuzi ya sakata la Akaunti ya Escrow, misaada mingine
iliyositishwa inahusu sekta ya maji na afya, ndiyo maana miradi mingi kwenye
Halmashauri sasa haisongi mbele,” alisema.
Mnyika alisema mkutano ujao wa bunge wataenda kuyaeleza kwa
kina kuhusu misaada hiyo ya maji na afya iliyositishwa.
“Leo tunapata madhara syo tu miradi ya kimaendeleo kukwama,
wananchi wanakosa huduma muhimu za afya na maji kwa sababu ya fedha kutumika
kwenye mianya ya ufisadi badala ya maendeleo,) “ alisema na kuongeza:
“Ukosefu huu wa fedha umeathiri pia tume katika zoezi muhimu
kwa ajili ya uchaguzi utakaowawezesha Watanzania kupata viongozi bora na kuzuia
mianya ya ufisadi,” alisema.
Alisema kitendo cha Jaji Lubuva kuvinyamazisha vyama vya
siasa wakati BVR zina upungufu ni sawa na funika kombe mwanaharamu apite.
Mnyika alisema chama chake kitaendelea kuzungumzia udhaifu
na upungufu huo ambao mwisho unaweza kusababisha watu kuandikishwa zaidi ya
mara moja.
Alisema endapo watanyamaza nchi itaingia katika machafuko kwa
kuwa upungufu uliopo kwenye mashine hizo ni mkubwa.
“Kuacha kujadili suala hili nchi itaingia katika hasara ya
kutumia fedha kwenye uandikishaji wakati huo, hii ni kuruhusu mianya ya
uchakachuaji wa uchaguzi na kusababisha kutokuwa huru na haki,” alisema.
Aidha chama hicho kimeonyesha wasiwasi wa kutokamilika kwa
zoezi la uandikishaji mwezi Aprili 30 kama ilivyotakiwa kutokana na siku ambazo
zitakazotumika kila mkoa.
“Lubuva amesema Njombe watatumia siku 28 wasiwasi wetu ni kwamba ikiwa siku hizi zitatumika
na maeneo mengine, itafika Aprili 30, baadhi ya maeneo yatakuwa hayajakamilisha
zoezi,” alisema.
Aidha, kutokana na wasiwasi huo, wamemtaka Rais Jakaya
Kikwete asogeze mbele hadi uchaguzi mkuu utakapomalizika ndipo lifanyike.
Pia Mnyika amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda aeleze lini
kamati ya bunge itakutana na Tume ili kuepusha nchi kuingia katika machafuko.
Kuhusu kauli ya Tume ya kuvitaka vyama vya siasa kusaidia
kutoa elimu uandikishaji kwa wananchi, Mnyika alisema chama chake kimeitikia
wito huo na kina kusudia kwenda mkoani Njombe kuzindua kampeni ya elimu ya
mpiga kura maarufu kama ‘R to R BVR’
ikimaanisha Region to Region BVR. Hata hivyo, alisema baada ya kupeleka taarifa
jeshi la polisi kuhusiana na mkutano wa uzinduzi huo, wamekataliwa kufanya
hivyo kwa maelezo kuwa kutakuwa na zoezi la uandikishaji huo.
Alisema licha ya polisi kuzuia lakini wataendelea na zoezi
hilo na kumtaka Mkuu wa jeshi hilo awaagize polisi kupokea mikutano hiyo ambayo
imekusudiwa kufanyika kila mkoa.