ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Telesphor Mkude amewataka wanandoa kuachana na jambo la talaka kwa kuwa limekuwa likiathiri maisha ya familia hasa ustawi wa watoto.
Askofu Mkude aliyasema hayo Jumapili iliyopita kabla ya kutoa kipaimara kwa watoto 160 wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrick la mjini hapa. Alisema kuwa wanandoa wanapaswa kuuishi upendo wa Yesu kwa kuwa upendo huo hauna talaka na kufafanua kuwa mwanaume anapaswa kumpenda mke huku mwanamke akitakiwa vile vile kumpenda na kumtii mumewe kwa upendo ule ule wa Kristo Yesu.
“Utakatifu wetu ni katika kuishi kama Kristo alivyolipenda kanisa lake, baba mpende mkeo na mama mpende mumeo kama Kristo alivyolipenda kanisa lake,” alisisistiza Askofu Mkude.
Hivyo aliwataka wanandoa kuendelea kutunza viapo vyao siku walipofunga ndoa zao. Alisema ndoa inaposambaratika wanaoumia ni watoto ambapo alisema kuwa wazazi wanatakiwa kuwa mfano mzuri kwa watoto wao kwa kutoingiza sura ya talaka kwenye ndoa.
Aidha aliwataka wazazi kutambua miito ya watoto wao ikiwa ni pamoja na kuiheshimu. Alisema kuwa wazazi wengi wamekuwa wakiwakatisha tamaa watoto kwa kuwachagulia wito, jambo ambalo alisema linamfanya mtoto ashindwe kuishi kwa amani.
Hivyo aliwataka waumini hao kuhakikisha wanatunza utakatifu walioupata siku ya ubatizo kwa kuhakikisha kitambaa cha roho zao kikiwa kisafi kwa kumshirikisha Roho Mtakatifu ambaye ndiye mtakasaji.
 
Top