DAR ES SALAAM: Imefichuka!  Kifo cha Askofu wa Kanisa la Taliteha, Ubungo jijini Dar, Fred Mwarusi (45) kilichotokea chumbani kwake, Makuburi, Jumapili iliyopita kimezua mengi na mazito, Chanzo chetu kimefuatilia kwa kina.

Mwili wa marehemu huyo ulibainika na majirani baada ya kusikia harufu kali kutokea kwenye chumba chake kutokana na kutomwona akiingia wala kutoka kwa siku kadhaa.

 Kwa mujibu wa chanzo makini, kabla ya kifo chake, Askofu Mwalusi alijifungia chumbani mwake kwa siku kadhaa nyuma kwa ajili ya kufanya maombi ya uponyaji kwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua ambayo hayajajulikana mara moja.
“Askofu Mwalusi alikuwa akisumbuliwa na maradhi f’lani hivi, yalimfanya afya yake kudhoofu. Majirani zake na  waumini wake walimshauri mara kwa mara kwenda kutibiwa hospitali ili arejeshe afya yake, lakini alikuwa akigoma kwa maelezo kwamba, atafanya maombi, atapona kwa Jina la Yesu.

“Alikuwa akisema dawa pekee kwenye matatizo yake ya kiafya ni maombi tu na kuonesha kuwashangaa sana waliokuwa wakimshauri habari ya kwenda hospitali,” kilisema chanzo.

 Akizungumza na chanzo chetu juzi kwenye msiba wa askofu huyo, mmoja wa majirani zake aliyekataa katakata jina lake kuandikwa gazetini, alisema siku ya mwisho kumuona marehemu huyo ilikuwa Ijumaa ya Julai 29, mwaka huu ambapo aliingia ndani kwake halafu akasikika akifanya maombi kwa kumuomba Mungu ampe afya njema.
“Nilimsikia akimwomba Mungu ampe afya njema. Lakini baada ya maombi hayo ya nguvu, nikamsikia akikemea pepo kwa sauti ya chini sana kisha sikumsikia tena mpaka leo (Jumapili) ndiyo tukaanza kusikia harufu ikitoka chumbani.”
WASIWASI ULIANZA
“Lakini kuna wakati tuliingiwa na wasiwasi kwa kutomuona mwenzetu akifungua mlango wake tangu Ijumaa jambo ambalo halikuwa la kawaida kwake. Alikuwa mtumishi wa Mungu mwenye harakati za kiroho kila wakati, akiingia na kutoka, pengine akiwa anaimba nyimbo mbalimbali.”

 “Kufuatia hali hiyo, tuliambizana kuwa tupige simu polisi ambao walifika hapa na kuvunja chumba chake, wakamkuta amefariki dunia,” alisema jirani huyo.

Akizungumzia tukio hilo Jumatatu iliyopita, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makuburi Kibangu, Moshi Kaftani alisema alipewa taarifa za kifo cha mtumishi huyo wa Mungu na mmiliki wa nyumba, Peter Mrema ambapo alishirikiana na polisi kuvunja mlango na kumkuta ameshafariki dunia huku kukiwa na harufu kali chumbani humo.
“Huyu marehemu ni mwananchi wangu ambaye alikuwa askofu na baadhi ya waumini wake ni wale pale unaowaona na wachungaji wake walikuwepo hapa lakini sasa hivi wameshaondoka.”
 
MZOZO WA MAZISHI?
Juzi Jumanne, kulidaiwa kuibuka kwa mzozo wa eneo sahihi la kumzikia marehemu huyo ambapo, baadhi ya ndugu walisema asafirishwe kwenda Mbeya lakini mama wa marehemu akisema azikwe jijini Dar. Hata hivyo, mwenyekiti wa serikali ya mtaa alikanusha kuwepo kwa mzozo.
Mwili wa marehemu ulizikwa Jumanne iliyopita kwenye Makaburi ya Ubungo Maji jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na waumini wake, majirani na wachungaji huku ibada ya mazishi ikiongozwa na Askofu David Mwasota wa Kanisa la Naioth Gospel Assembly la jijini Dar.

KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo bila kufafanua zaidi.

 
Top